Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tumejiandaa kukabiliana na chokochoko za maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128342
Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haina imani na usitishaji vita uliopo, na kwamba imejiandaa kukabiliana na senario tofauti za uchokozi wa maadui.
(last modified 2025-07-15T06:23:22+00:00 )
Jul 15, 2025 04:34 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tumejiandaa kukabiliana na chokochoko za maadui

Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haina imani na usitishaji vita uliopo, na kwamba imejiandaa kukabiliana na senario tofauti za uchokozi wa maadui.

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh ameyasema hayo katika mazungumzo mawili tofauti ya simu aliyofanya na mawaziri wenzake wa Uturuki na Malaysia jana Jumatatu.

"Jamhuri ya Kiislamu haitaki kueneza vita na ukosefu wa usalama katika eneo hili, lakini iko tayari kujibu kwa uthabiti na kwa nguvu zote vitendo vyovyote vya kichokozi vya wavamizi," Jenerali Nasirzadeh amemwambia Waziri wa Ulinzi wa Uturuki.

Ameongeza kuwa,"Jamhuri ya Kiislamu haina imani na usitishwaji wa mapigano. Kwa hiyo, imetabiri na kujiandaa kujibu senario mbalimbali za uchokozi mpya."

Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yaşar Güler kwa upande wake amepongeza na kuelezea kuridhishwa kwake na usitishwaji mapigano akieleza kuwa, "Tunaamini kuwa mazungumzo ya nyuklia yanapaswa kuhitimishwa kwa makubaliano faafu ambayo yatanufaisha Iran na eneo zima."

Brigedia Jenerali Nasirzadeh aidha katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Malaysia, Mohamed Khaled Nordin, ameishukuru serikali ya Kuala Lumpur kwa misimamo yake thabiti ya kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kidhalimu na vya kutwishwa vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel na Marekani dhidi ya taifa hili.

Waziri wa Ulinzi wa Malaysia kwa upande wake amesema kuwa Iran ni nchi rafiki na ya kutegemewa kwa Malaysia na kuongeza kuwa, "Tunailaumu Israel kwa vita hivyo, na ndiyo maana tuliyaani vikali mashambulizi hayo tangu mwanzo."