Putin: Migongano kati ya Russia na Magharibi haihusiani na idiolojia
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema malengo ya kiukiritimba ya mataifa ya Magharibi na kutupilia mbali kwao wasiwasi wa kiusalama wa nchi yake ndivyo vilivyosababisha mzozo unaoendelea hivi sasa kati ya Moscow na Magharibi.
Putin amesisitiza kuwa, tofauti za kiidiolojia ni kisingizio tu kinachotumiwa kufanikisha maslahi ya kijiopolitiki ya Magharibi.
Rais wa Russia ameongeza kuwa alitegemea kwamba kuanguka kwa shirikisho la Urusi ya zamani USSR kungepunguza mvutano kati ya Russia na Magharibi.
"Pia nilifikiri kwamba mabishano makuu [kati yetu] yalikuwa ya kiitikadi," ameeleza Putin na kuongezea kwa kusema: "pamoja na hayo, hata wakati Umoja wa Kisovieti ulipotoweka ... mbinu ya kuyatoa maanani maslahi ya kimkakati ya Russia iliendelea."
Rais wa Russia ameendelea kueleza kwamba jitihada zake za kuwabainishia viongozi wa Magharibi wasiwasi wa Russia ziliambulia patupu. "Magharibi waliamua kuwa hawahitaji kufuata sheria inapohusu Russia, ambayo haina nguvu sawa na USSR."
Amesisitiza kuwa kilichodhihirika ni kwamba, bila ya Russia kujiweka katika nafasi ya kuwa taifa huru linalojitawala, halitazingatiwa na kuheshimiwa.
Moscow imetaja masuala kadhaa ikiwemo matashi liliyonayo shirika la kijeshi la NATO kwa Ukraine na usaidizi wa kijeshi wa Magharibi kwa nchi hiyo kuwa sababu kuu za mzozo wa kijeshi unaoendelea nchini Ukraine. Kabla ya kupamba moto hali hiyo mapema mwaka 2022, Russia ilitaka ushughulikiwe wasiwasi wa kiusalama ilionao kwa kupatiwa dhamana na Marekani na NATO, na vile vile kuhakikishiwa kuwa Ukraine haitafungamana na upande wowote lakini matakwa yake hayo yalikataliwa na Magharibi.../