Kwa nini Trump amemwekea vikwazo Rais wa Cuba?
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza vikwazo vipya vya fedha dhidi ya Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel na maafisa wengine waandamizi wa nchi hiyo pamoja na marufuku ya usafiri kwa kisingizio cha kukandamiza maandamano ya amani yaliyofanyika mwaka 2021.
Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amedai kuwa, miaka minne nyuma, maelfu ya raia wa Cuba walimiminika mabarabarani na kuandamana kwa amani kudai mustakabali usio na udikteta, lakini utawala wa Cuba ulikabiliana na maandamano hayo kwa ukatili na ukandamizaji mkubwa na kuwaweka kizuizini watu wengi kinyume cha sheria. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani sasa inachukua hatua kadhaa za kutekeleza sera zilizoongezwa msukumo za serikali ya Trump kuhusiana na Cuba, ili kuonyesha mshikamano na watu wa Cuba na wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo.
Vikwazo vipya vya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani dhidi ya Rais wa Cuba Miguel Díaz-Canel na maafisa wengine waandamizi wa Havana kwa mara nyingine tena vimeongeza mvutano katika uhusiano wa nchi hizo mbili; na hatua hiyo iliyochukuliwa kwa madai ya kukandamizwa wananchi walioandamana kwa amani mwaka 2021, inaakisi tena utekelezwaji wa sera ambayo chimbuko lake ni historia ndefu ya uhasama, ushindani wa kiitikadi, na makabiliano ya kijiopolitiki baina ya nchi hizo mbili.

Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, uhusiano kati ya Marekani na Cuba umekuwa moja ya mahusiano tata zaidi na yenye mvutano mkubwa zaidi ya kidiplomasia katika upande wa magharibi wa sayari ya dunia. Chanzo cha mivutano hiyo ni Mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959 na kuenea Ukomunisti katika eneo jirani na Marekani, jambo ambalo liliitia wasiwasi Washington wa kuenea ushawishi wa Urusi na kusambaa itikadi ya kikomunisti katika eneo hilo. Baada ya Mapinduzi ya Cuba, Marekani iliiwekea Cuba vikwazo vikali vya kiuchumi na kidiplomasia kwa visingizio mbalimbali, vikwazo ambavyo vimekuwa vikiendelea hadi sasa kwa tofauti tu ya kuongezwa au kupunguzwa makali yake. Katika miaka ya hivi karibuni, sera za vikwazo vya Washington dhidi ya Cuba zimekuwa zikiimarishwa mara kwa mara kwa kisingizio cha ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa wapinzani, na kila mara zimekuwa zikikabiliwa na mijibizo mikali ya viongozi wa Cuba.
Vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Cuba vinawekwa na kutekelezwa katika hali ambayo viongozi wa Havana wamekuwa wakivilaani na kuvielezea kuwa ni “hujuma na mzingiro wa kiuchumi” unaoilenga nchi yao. Kwa mujibu wa viongozi hao, vikwazo hivi vimewaadhibu watu wote wa Cuba na ni kizuizi kikubwa kwa maendeleo ya nchi hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodriguez ameielezea sera hiyo ya Washington kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu za wananchi wote wa Cuba. Katika jibu alilotoa kwa hatua ya karibuni zaidi ya serikali ya Trump dhidi ya Cuba, Rodriguez ameandika katika mtandao wa kijamii wa X: "suala hili limezipa nguvu zaidi hujuma na mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Cuba na kuwaadhibu watu wote wa Cuba, na hiki ni kizuizi kikuu kwa maendeleo. Hii ni tabia ya kihalifu ambayo inakiuka haki za binadamu za taifa zima."
Viongozi wa Marekani wanajifanya watetezi wa haki za binadamu katika hali ambayo, kwa upande wa nje ya nchi, hatua ya kuiwekea Cuba vikwazo vya kiuchumi, hasahasa katika sekta ya bidhaa za chakula na dawa, ni ukiukaji wa haki za binadamu; na kwa upande wa masuala ya ndani ya Marekani kwenyewe watawala wa Washington wanakanyaga pia haki za binadamu za raia wao. Kuwaadhibu wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopinga sera za Washington za kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel, na namna maafisa wa Washington wanavyowatendea wahajiri na kuwatimua nchini humo ni mifano ya wazi inayothibitisha kuwa kaulimbiu ya kutetea haki za binadamu inayopigiwa upatu na viongozi wa Marekani si chochote zaidi ya porojo tu. Kuhusiana na suala hilo, kumuwekea vikwazo rais wa Cuba kwa kisingizio cha ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa miaka minne iliyopita nako pia kunapasa kuchukuliwe kuwa ni sehemu ya sera za Marekani za kuishinikiza serikali ya Cuba na kuizuia nchi hiyo isiimarishe uchumi wake bila ya utegemezi na ufuataji wa siasa na sera za Washington.../