Iran: Tutatoa jibu mwafaka iwapo tutarejeshewa vikwazo vya UN
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amesema jaribio lolote la kuanzisha kile kinachoitwa utaratibu wa kurudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hili ni sawa na hatua ya makabiliano ambayo itapokea jibu mwafaka kutoka Tehran.
"Kwa kuzingatia maendeleo ya hivi majuzi, kugeukia utaratibu wa kurejesha (vikwazo) hakuna msingi na hakuna mashiko ya kisheria, kisiasa na kimaadili zaidi kuliko hapo awali," Baghaei alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari wa kila wiki mjini Tehran jana Jumatatu.
Ameongeza kuwa, utaratibu huo ni utekelezaji tu wa kifungu ambacho kilijumuishwa katika Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo linaidhinisha makubaliano ya nyuklia ya 2015, na hakina uhalali wowote.
Amesisitiza kuwa, Iran ingali mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na ilipunguza ahadi zake tu kwa kujibu ukiukaji mkubwa wa pande nyingine wa majukumu yao yaliyoainishwa katika makubaliano ya nyuklia, ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa amesema kuwa Troika ya Ulaya, yaani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kwa kuunga mkono vitendo vya uchokozi vya utawala wa Israel dhidi ya Iran kwa kisingizio kuwa Iran inataka kuunda silaha za nyuklia. Amebainisha kuwa, Iran haijapokea waraka rasmi kuhusu uamilishwaji wa utaratibu wa kuhuisha vikwazo dhidi ya taifa hili (snapback).
Gharibabadi amesema Iran bado haijapokea taarifa rasmi kwamba Umoja wa Ulaya unanuia kufufua utaratibu huo wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, lakini wanatarajia kufanya hivyo siku moja.