Esmaeil Baqaei: Iran yasema haitakubali ubabe wa Marekani katika mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137848-esmaeil_baqaei_iran_yasema_haitakubali_ubabe_wa_marekani_katika_mazungumzo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesisitiza kuwa Iran ilikataa mapendekezo aliyoyaita “yasiyo na mantiki” yaliyowasilishwa na Marekani katika mazungumzo yaliyofanyika Islamabad, akionya kuwa Tehran haitawahi kukubali mazungumzo yanayoendeshwa kwa mfumo wa ubabe na kulazimisha masharti.
(last modified 2026-04-16T06:12:26+00:00 )
Apr 16, 2026 06:05 UTC
  • Esmaeil Baqaei: Iran yasema haitakubali ubabe wa Marekani katika mazungumzo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesisitiza kuwa Iran ilikataa mapendekezo aliyoyaita “yasiyo na mantiki” yaliyowasilishwa na Marekani katika mazungumzo yaliyofanyika Islamabad, akionya kuwa Tehran haitawahi kukubali mazungumzo yanayoendeshwa kwa mfumo wa ubabe na kulazimisha masharti.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kila wiki siku ya Jumatano, Baqaei amesema kuwa ubadilishanaji wa taarifa kupitia upatanishi wa Pakistan umeendelea tangu Jumapili iliyopita, na kwamba misimamo ya Iran iko wazi na tayari imewasilishwa.

Ametangaza pia kuwa Iran ujumbe wa maafisa kutoka Pakistan umefika Tehran ili kujadili kwa kina mitazamo ya pande zote mbili, yaani Iran na Marekani, kama mwendelezo wa mazungumzo ya Islamabad.

Msemaji huyo alisisitiza kuwa kwa sasa Pakistan ndiyo nchi pekee inayofanya upatanishi katika kubadilishana taarifa kati ya Iran na Marekani.

Akizungumzia mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Iran na Marekani mjini Islamabad, Baqaei amesema safari hii lengo lilikuwa kusitishwa kabisa kwa vita na kupatikana kwa haki za Iran, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo na fidia kwa hasara zilizosababishwa na vita vilivyolazimishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Baqaei amesisitiza kuwa Iran haitaingia kwenye mazungumzo kwa lengo la kukubali masharti ya Marekani, akiongeza kuwa kipimo kikuu kinachoongoza timu ya mazungumzo ni maslahi na haki za taifa la Iran.

Amefanua kuwa iwapo mazungumzo yatategemea upande mmoja kulazimisha masharti yake kwa upande mwingine, basi hilo si mazungumzo bali ni kulazimishwa na kuamrishwa, jambo ambalo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitalikubali kamwe.

Akijibu madai ya Makamu wa Rais wa Marekani kwamba mapendekezo rahisi na ya jumla yaliwasilishwa kwa Iran katika mazungumzo ya Islamabad, Baqaei amesema Iran iliwasilisha mpango wake wa vipengele kumi kama jibu kwa mpango wa Marekani uliodaiwa kuwa na vipengele kumi na tano.

Aliongeza kuwa katika mpango huo, Iran ilieleza wazi misimamo yake kuhusu masuala yote ya mazungumzo, ikiwemo suala la nyuklia, kuondolewa kwa vikwazo, fidia ya hasara na kusitishwa kwa vita.

Alipoulizwa kuhusu pendekezo la Russia la kuhamisha urani iliyorutubishwa ya Iran kwenda Moscow, Baqaei ameema kuwa katika makubaliano yoyote ya nyuklia kuna chaguo mbalimbali zinazoweza kuzilngatiwa.