Jenerali Mousavi: Makombora ya Iran yalikata mikono ya maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128316
Kamanda mkuu wa Jeshi la Iran amevipongeza vikosi vya anga vya nchi hii kwa mashambulio madhubuti ya makombora waliyoyafanya dhidi ya maadui wa taifa hili mwezi uliopita na kuonya kwamba, kosa lolote litakalorudiwa litakabiliwa kwa jibu kali zaidi.
(last modified 2025-07-15T02:36:31+00:00 )
Jul 14, 2025 12:43 UTC
  • Jenerali Mousavi: Makombora ya Iran yalikata mikono ya maadui

Kamanda mkuu wa Jeshi la Iran amevipongeza vikosi vya anga vya nchi hii kwa mashambulio madhubuti ya makombora waliyoyafanya dhidi ya maadui wa taifa hili mwezi uliopita na kuonya kwamba, kosa lolote litakalorudiwa litakabiliwa kwa jibu kali zaidi.

Kamanda Mkuu wa Makao Makuu ya Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, alitoa kauli hii leo Jumatatu, alipotembelea vituo na askari wa Kikosi cha Wanaanga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

"Ulikuwa upanga mkali uliotumiwa na Kikosi cha Aanga ambao, kupitia usaidizi wa Kimungu, uliweza kukata vichwa vya maadui na mikono yao," kamanda huyo amesema.

Mashambulizi makali ya anga ya Israel yalilenga Jamhuri ya Kiislamu kati ya Juni 13 na 25, na kuilazimisha nchi hii kuanza mashambulizi ya haraka na ya nguvu ya kujibu mapigo.

Kamanda Mousavi amesema kulipiza kisasi kwa Kikosi cha Wanaanga kulizidi kwa mbali mashambulizi yake wakati wa vita vya kutwishwa vilivyoanzishwa na Iraq katika miaka ya 1980.

Mejan Jenerali Mousavi amelihakikishia taifa zima la Iran kwamba, "ikiwa adui atafanya kosa jingine, wanajeshi wetu watasimama imara kutoa jibu la kujutisha na lenye nguvu zaidi."

Amesisitiza kuwa, Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu vilikabiliana na uvamizi wa Israel na Marekani kwa nguvu na uwezo kamili wa kijeshi wakati wa mashambulizi ya kichokozi ya mwezi uliopita ya Tel Aviv na Washington.

Jenerali Mousavi amesema kuwa, vita vya kutwishwa vya siku 12 vilithibitisha uhalali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwani Vikosi vya Ulinzi vya nchi hii vilikabiliana na uonevu na uchokozi kwa nguvu zote.