Rais Gustavo Petro: Colombia lazima ivunje uhusiano wake na NATO
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128442-rais_gustavo_petro_colombia_lazima_ivunje_uhusiano_wake_na_nato
Rais Gustavo Petro wa Colombia amesema nchi yake inapaswa kukata uhusiano wake na NATO kwa kuwa viongozi wa shirika hilo la kijeshi la Magharibi wanaunga mkono "mauaji ya halaiki" ya Wapalestina.
(last modified 2025-10-16T03:06:03+00:00 )
Jul 17, 2025 14:02 UTC
  • Rais Gustavo Petro: Colombia lazima ivunje uhusiano wake na NATO

Rais Gustavo Petro wa Colombia amesema nchi yake inapaswa kukata uhusiano wake na NATO kwa kuwa viongozi wa shirika hilo la kijeshi la Magharibi wanaunga mkono "mauaji ya halaiki" ya Wapalestina.

Colombia, mshirika wa jadi wa Marekani huko Amerika Kusini, ilikuwa nchi ya kwanza katika eneo hilo kupata hadhi ya mshirika wa kimataifa wa NATO mwaka 2017. Petro, ambaye aliingia madarakani mwaka 2022 kama rais wa kwanza wa mrengo wa kushoto wa Colombia, alivunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka jana kutokana na kile anachoeleza kuwa mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina.

"Tunafanya nini katika NATO? Ikiwa viongozi wa juu wa NATO wanaunga mkono mauaji ya kimbari, tunafanya nini huko?" Petro alisema katika mkutano wa kimataifa unaoiunga mkono Palestina mjini Bogota.

Matamshi ya Rais wa Colombia yamekuja huku muungano wa mataifa mbalimbali duniani yaliyokutana Bogota, mji mkuu wa Colombia kukubaliana kutekeleza hatua sita za kukomesha mashambulizi ya utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza na kuzuia ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala huo haramu.

"Tumekuja Bogota kuweka historia - na tumeiweka," ameeleza Rais wa Colombia Gustavo Petro, katika "mkutano wa dharura" ulioandaliwa kwa pamoja na serikali za Colombia na Afrika Kusini kama wenyeviti wenza wa Kundi la The Hague, ili kuratibu hatua za kidiplomasia na za kisheria kukabiliana na kile wanachoelezea kama "kinga ya kutofuatiliwa kisheria" inayowezeshwa na Israel na washirika wake wenye nguvu.