Ghalibaf: Majeshi ya Iran yataendelea kuwaadhibu wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137182-ghalibaf_majeshi_ya_iran_yataendelea_kuwaadhibu_wavamizi
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Bagher Ghalibaf amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza operesheni zake za kulipiza kisasi mpaka ihakikishe imewaadhibu vya kutosha na kuwatia adabu wavamizi walioanzisha chokochoko dhidi ya taifa hili.
(last modified 2026-03-05T10:52:08+00:00 )
Mar 05, 2026 10:52 UTC
  • Ghalibaf: Majeshi ya Iran yataendelea kuwaadhibu wavamizi

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Bagher Ghalibaf amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza operesheni zake za kulipiza kisasi mpaka ihakikishe imewaadhibu vya kutosha na kuwatia adabu wavamizi walioanzisha chokochoko dhidi ya taifa hili.

Ghalibaf amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa, Iran itaendelea kutoa vipigo kwa wavamizi, licha ya makanda wa jeshi la Marekani kutozungumza chochote kuhusu mashambulizi ya kulipiza kisasi ya majeshi ya Iran ambayo yameisababishia hasara kubwa Washington.

Maafisa wa Iran wamesema kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani anapaswa kutarajia gharama kubwa zaidi baada ya zaidi ya wanajeshi 500 wa Marekani kuuawa katika siku chache za kwanza za vita vyao vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Spika wa Bunge la Iran amebainisha kuwa: Maafisa wa Marekani wameiambia Kongresi kuwa hawajaandaa mpango wa kujiondoa kwenye vita, lakini katika vyombo vya habari wanajipiga kifua ili kujaribu kudhibiti masoko (ya hisa).

Ghalibaf ameashiria mashambulizi yanayoendelea ya utawala wa Israel na Marekani dhidi ya taifa hili na kueleza kuwa, operesheni za Iran zinazolenga milki na maeneo ya Marekani na Israel katika eneo zimeonyesha uwezo wa uendeshaji na mshikamano, na kuwashangaza wachambuzi wa masuala ya kijeshi.

Kituo mashuhuri cha utafiti cha Marekani, CPA kimefichua kuwa, vita vya kichokozi dhidi ya Iran vimeisababishia hasara kubwa Marekani na kwamba mbali na kuuawa idadi kubwa ya wanajeshi wa nchi hiyo, hadi tarehe 3 Machi, yaani katika siku tatu za vita hivyo, Marekani ilikuwa imepata hasara ya dola bilioni 5 za walipakodi wa nchi hiyo.