Larijani: Iran haitajadiliana chochote na makundi yanayotaka kujitenga
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitafanya majadiliano wala mazungumzo yoyote na makundi yanayotaka kujitenga.
Ali Larijani amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X, ambapo ameyaonya vikali makundi hayo. Dakta Larijani amesema: Majeshi yetu yenye nguvu yana ufahamu juu ya jambo hilo (la makundi yanayotaka maeneo yao yajitenge na Iran), na katu Iran haitaruhusu jambo hilo kufanyika.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameeleza bayana kuwa, vikosi vya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu vitachukua hatua yoyote faafu kuzima nyendo na harakati za makundi hayo.
Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa wa Marekani kudai kuwa, serikali ya Donald Trump iko tayari kuyapa silaha makundi ya Iran yanayotaka kujitenga. Kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, Iran ina haki ya kuendesha operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi wenye silaha wanaotaka kujitenga, wanaofanya mauaji na kuvuruga usalama wake.
Vikosi vya makombora na ndege zisizo na rubani za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu vimekuwa vikilenga makao makuu ya makundi ya kigaidi ya Komoleh na Democratic katika mikoa ya Sulaymaniyah na Erbil nchini Iraq. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, inafahamu vyema kuwa makundi hayo ya kigaidi yanaungwa mkono na utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za kibeberu ikiwemo Marekani.
Nyayo za makundi hayo zilionekana wazi katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, ambapo yalitumiwa na Wamagharibi kuwashambulia na kuua shahidi maelfu ya Wairani wasio na hatia wakati wa maandamano ya mwezi Januari.