Jan 14, 2021 03:08 UTC
  • Mshauri wa Kiongozi Muadhamu: Marekani haiwezi kuihadaa Iran kwa pipi

Mshauri wa ngazi ya juu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani sharti iiondolee Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vyote na kwamba Tehran haitakubali kitu kingine ghairi ya hicho.

Ali Larijani amesema hayo katika mahojiano na tovuti ya khamenei.ir ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei na kuongeza kuwa: Naamini kuwa kamwe hawawezi kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iwapo hawataondoa vikwazo.

Larijani ambaye amewahi kuwa Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameeleza bayana kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni asilimia 100 kinyume na ahadi ilizotoa na kwa msingi huo hawawezi kurejea katika JCPOA bila kuondoa vikwazo hivyo.

Amesema ni jambo lisilokubalika wao kusema kuwa, 'tutarejea kisha tutajadiliana baadaye.' Dakta Larijani amebainisha kuwa, "Nukta ya msingi ni kufuta vikwazo vyote na hakuna shaka kuwa, iwapo hawataviondoa, kamwe hawawezi kurejea katika mapatano hayo kwa kuwa watakuwa wamefeli kutekeleza wajibu wao.   

Hatua ya Trump ya kuiondoa US katika JCPOA imeendelea kukosolewa ndani na nje ya Marekani

Mshauri wa ngazi ya juu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, ramani ya njia ya kutekeleza haya inahitajika, na iwapo Marekani inadhani kuwa itaihadaa Iran kwa chokoleti, hilo litaonyesha namna hawana umakinifu.

Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif aliiambia tovuti ya khamenei.ir kuwa, kurejea Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA bila Iran kuondolewa vikwazo ni kwa maslahi ya Washington na wala si kwa maslahi ya Tehran.

 

Tags