Malengo ya mashambulizi ya Marekani na Israel nchini Lebanon
Mashambulizi ya jeshi la Israel kwa kushirikiana na Marekani dhidi ya Lebanon yameingia katika awamu mpya.
Israel imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Lebanon na kukanyaga makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa baina ya pande mbili. Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Lebanon na utawala wa wa Kizayuni yalitiwa saini mwezi Novemba 2024, lakini Israel inaendelea kuthibitisha kivitendo kuwa si dola lenye mwamana, bali ni dola kidhabu na pandikizi ambalo haliheshimu hata kidogo makubaliano linayoyatia saini lenyewe.
Awamu hii mpya ya vita dhidi ya Lebanon imeanza katika hali ambayo makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano yamefikiwa pia kwenye Ukanda wa Ghaza. Jeshi la Israel kwa makubaliano na usimamizi wa moja kwa moja wa maafisa wa Marekani, limeamua kufanya mashambulizi mapya dhidi ya maeneo mbalimbali ya harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon. Sasa swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni nini malengo ya mashambulizi hayo mapya ya Marekani na Israel dhidi ya Lebanon?
Moja ya malengo makuu ya mashambulio hayo ni kuishinikiza serikali ya Lebanon na kujaribu ifuate mkondo wa kuipokonya silaha harakati ya Hizbullah. Serikali ya Lebanon huko nyuma ilisema kuwa itajitolea kuipokonya silaha Hizbullah ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2025, suala ambalo limekataliwa vikali na harakati ya Hizbullah ambayo muda wote inasema kuwa, silaha za harakati hiyo ni za kujihami na kuwalinda wananchi wa Lebanon mbele ya jinai za mara kwa mara za Israel. Sheikh Naim Qassem Katibu Mkuu wa Hizbullah na maafisa wengine wa harakati hiyo wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba kamwe hawatokubali kupokonywa silaha harakati hiyo. Jambo muhimu zaidi hapa ni kwamba, hivi karibuni, hata baadhi ya watu mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiarabu nao wamejitokeza na kupinga waziwazi kupokonywa silaha Hizbullah. Inaonekana ni kwa sababu hiyo ndio maana Israel kwa msaada wa pande zote wa Marekani, imeanza tena mashambulizi dhidi ya maeneo ya Hizbullah huko Lebanon.
Lengo jingine la mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel huko Lebanon ni kujaribu kuizuia Hizbullah kujenga upya nguvu zake za kijeshi. Utawala wa Kizayuni una wasiwasi kwamba Hizbullah itatumia fursa iliyopo kurejesha nguvu zake za kijeshi. Katika siku za hivi karibuni, kuna ripoti zimetolewa kuhusu suala hilo zikisema kwamba Hizbullahh inajenga upya nguvu zake za kijeshi na itaendelea kupambana na Israel kwa nguvu kubwa zaidi kuliko huko nyuma.
Hii ni kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umeamua kuhama kutoka kwenye mkakati wa kusubiri makubaliano ya kisiasa na umegeukia sera ya "mashinikizo ya kijeshi ya polepole" ili kulazimisha kufanyika kile unachotaka.
Lengo la tatu la mashambulizi haya linahusiana na hali ya ndani ya ardhi za Palestina zinzokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Katika vita dhidi ya Ghaza, licha ya Israel kufanya mauaji makubwa ya kimbari, Netanyahu ameshindwa kufikia malengo yake kupitia njia za kijeshi. Zaidi ya hayo, lengo la Israel la kuvunjwa au kupokonywa silaha Hamas nalo halijafikiwa.
Netanyahu hivi sasa yuko chini ya mashinikizo makubwa kutoka kwa kambi ya upinzani wa ndani ya Israel pamoja na baadhi ya washirika wake katika baraza lake la mawaziri. Hali kwa waziri mkuu huyo wa Israel ni mbaya kiasi kwamba hata kumekuwa na ripoti za uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa mapema wa bunge ukiashiria kuwadia mwisho wa maisha yake ya kisiasa.
Baadhi ya uchunguzi wa maoni pia unaonesha kupungua imani ya wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kwa chama cha Likud cha Netanyahu, pamoja na kupungua idadi ya viti ambavyo chama hicho kinavishikilia bungeni.
Hivyo, mashambulizi mapya dhidi ya Lebanon yanatokana pia na hali ya ndani ya utawala wa Kizayuni kwa Netanyahu mwenyewe ambaye anajaribu kulinda nafasi yake na ya chama cha Likud katika milingano ya kisiasa ndani ya Israel.
Mwanadiplomasia mmoja wa Kiarabu ameliambia gazeti la Al-Jumhuriya kwamba lengo kuu la kuongezeka mashambulizi mapya ya Marekani na Israel dhidi ya Lebanon si kuisambaratisha Hizbullah wala kuipokonya silaha, bali lengo hasa ni kumuokoa Netanyahu na mashinikizo ya ndani na kukilinda chama chake cha Likud kisisambaratike.
Hatari zaidi kwa Netanyahu ni kwamba baada ya kusitishwa mapigano huko Ghaza, sasa umefika wakati wa yeye kuburuzwa mahakamani. Jambo hilo limejitokeza kwa uwazi zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma. Kuna kila dalili za kuburuzwa kizimbani Netanyahu na kuhukumiwa kifungo jela. Kwa hivyo, nduli huyo wa Ghaza ameamua kufungua uwanja mpya wa mashambulizi ya kijeshi ili kuuzubaisha umma na kukimbia kesi, na kuna uwezekano vita dhidi ya Lebanon vitakuwa vikubwa zaidi madhali Netanyahu ataendelea kuhisi kuna hatari dhidi yake yeye mwenyewe binafsi.