Maduro: Marekani inalenga kupora mafuta, gesi na dhahabu ya Venezuela
https://parstoday.ir/sw/news/world-i132508-maduro_marekani_inalenga_kupora_mafuta_gesi_na_dhahabu_ya_venezuela
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, amesisitiza kuwa ulimwengu mzima unafahamu kuwa mabepari wanaotawala Marekani wanataka kupora mafuta, gesi na dhahabu ya nchi yake.
(last modified 2025-10-28T07:55:15+00:00 )
Oct 28, 2025 07:55 UTC
  • Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro
    Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, amesisitiza kuwa ulimwengu mzima unafahamu kuwa mabepari wanaotawala Marekani wanataka kupora mafuta, gesi na dhahabu ya nchi yake.

Amesema Marekani inadai kuwa inataka kuivamia Venezuela kwa ajili ya kukabiliana na  mihadarati lakini jambo ambalo liko wazi ni kuwa hakuna ukweli katika  madai yao na wanafahamu vyema nukta hiyo.

Ameeleza kuwa taifa lake lina hifadhi kubwa zaidi ya mafuta ya petroli duniani, na hakuna mwenye uwezo wa kuiondoa Venezuela katika mlingano wa kimataifa wa nishati.

Maduro pia ametangaza kuwa operesheni kadhaa zimefanyika kwa ajili ya kuwakamata mamluki waliokuwa na uhusiano na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).

Aidha, Rais huyo amemshutumu Waziri Mkuu wa Trinidad na Tobago kwa “njama na uchochezi wa vita,” akisema kuwa hatua hiyo inatokana na “udhaifu wa kibinafsi, kimwili, kiakili na kimaadili.”

Ameongeza: “Lengo lao ni kubadilisha utawala wa Venezuela ili kuiba mafuta, gesi na dhahabu.”

Akizungumzia shinikizo kutoka nje, Maduro amesema: “Sasa ni wakati wa kuchagua—tusimame na wanaopenda vita, kifo na ghasia, au tusimame na uhai.”

Kutokana na vitisho vilivyopo, amesema amekubali kufuta makubaliano yote ya nishati kati ya Venezuela na Trinidad na Tobago, pamoja na athari zote za kisheria zinazohusiana.

Trinidad na Tobago, inayopakana na Venezuela imetangaza kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Marekani.

Hivi karibuni Marekani ilituma meli ya kivita ya kubeba ndege, USS Gerald R. Ford , ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani,  pamoja na meli zingine tano za kivita kwenda Amerika ya Kusini, hatua ambayo imekosolewa vikali na Venezuela ikiitaja kuwa ya kichokozi, hatarishi, na kinyume cha sheria za kimataifa.

Tangu Septemba, Washington imeendesha mashambulizi kadhaa dhidi ya meli za kiraia na za uvuvi katika Bahari ya Karibiani, ikidai zinahusiana na biashara ya dawa za kulevya bila kutoa ushahidi wowote.