Uchaguzi wa mapema unafanyika Zanzibar leo
Leo, visiwa vya Zanzibar vimeingia katika hatua muhimu ya mchakato wa uchaguzi kwa kuanza rasmi zoezi la kupiga kura ya mapema, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika kesho, Oktoba 29, katika Tanzania Bara na visiwani.
Katika kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar, Rais wa sasa Dk. Hussein Ali Mwinyi anawania muhula mwingine kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akichuana na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, anayewakilisha ACT Wazalendo, chama cha upinzani ambacho kimekuwa kikikosoa vikali uamuzi wa kuendesha kura ya mapema.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), vituo vya kupigia kura ya mapema vimefunguliwa saa 1:00 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki na vinatarajiwa kufungwa saa 10:00 jioni. Matokeo ya urais yanatarajiwa kutangazwa ndani ya kipindi cha saa 72 baada ya kufungwa kwa vituo.
Akizungumza katika kikao na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje kilichofanyika Makao Makuu ya ZEC Maisara, Mwenyekiti wa Tume, Jaji George Joseph Kazi, alisema vifaa vyote vya kupigia kura vimewasilishwa katika ofisi za wilaya tayari kwa zoezi hilo. Baadhi ya maafisa wa ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa tume watapiga kura katika vituo 50 Unguja na Pemba. Amesema Kura ya mapema ni kwa mujibu wa sheria, na inalenga kurahisisha ushiriki wa watumishi wanaohusika na usimamizi wa uchaguzi siku ya Oktoba 29."
Wangalizi wametakiwa kutoingilia kazi za tume, na wafuate sheria na muongozo wa uangalizi. Zoezi hili linakuja baada ya kampeni za uchaguzi zilizodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja, tangu zilipoanza rasmi tarehe 11 Septemba, kukamilika jana Oktoba 27, huku vyama vikuu vikitoa ahadi na mikakati mbalimbali kwa wananchi wa Zanzibar.