Apr 18, 2020 03:04 UTC
  • Larijani: Iran itaendelea daima kutetea haki za wananchi madhulumu wa Palestina

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea daima kutetea haki za wananchi madhulumu wa Palestina.

Ali Larijani ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na kwa nyakati tofauti na Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati wa Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina.

Kwa nyakati tofauti, Ismail Haniya, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas na Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami ya Palestina jana waliwasiliana kwa njia ya simu na Spika wa Bunge la Iran ili kumjulia hali baada ya kupata maambukizi ya virusi vya corona na kumuombea dua apate afueni na uzima kamili. Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wa harakati za muqawama za Palestina walisema, Dakta Larijani ni miongoni mwa watetezi na waungaji mkono wa kudumu wa muqawama katika eneo.

Kutoka kushoto: Ziyad al-Nakhalah, Ali Larijani na Ismail Haniya

Katika mazungumzo aliyofanya na Ismail Haniya, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemshukuru kwa kumjulia hali na kueleza kwamba, wakati dunia inataabika kulikabili janga la corona, utawala wa Kizayuni umezidi kuthibitisha dhati yake halisi ya kutokuwa na utu kwa kuendelea mpaka hivi sasa kuuwekea mzingiro Ukanda wa Gaza; na kwa upande wa utawala wa Marekani, ushahidi bora zaidi unaofichua dhati yake ya kutokuwa na ubinadamu ni kuendeleza vikwazo vyake dhidi ya Iran.

Dakta Larijani amesema, inapasa Wapalestina wadumishe mshikamano wao kikamilifu kwa kutumia fursa na uwezo wao wote wa kisheria na wa rasilimaliwatu kukabiliana na hatua za kijinai za Wazayuni na akasisitiza kwamba, dunia ya baada ya corona ni fursa ya kuangaliwa upya haki za mataifa na utambulisho wa kiutu; na mfumo wa ubeberu unapaswa kujifunza na kupata somo la kubadilisha tabia na mwenendo wake kutokana na majanga ya kibinadamu.

Katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, ana matumaini kuwa mujahidina wa kambi ya muqawama wa Kiislamu watapata ushindi haraka katika mapambano na utawala wa Kizayuni.../

Tags