Washington Post: Makumi ya makombora ya Iran yameharibu vituo vya kijeshi vya Israel
(last modified Sun, 06 Oct 2024 02:51:12 GMT )
Oct 06, 2024 02:51 UTC
  • Washington Post: Makumi ya makombora ya Iran yameharibu vituo vya kijeshi vya Israel

Gazeti la Marekani la Washington Post limetangaza katika ripoti yake kwamba makumi ya makombora ya Iran yaliyorushwa siku ya Jumanne kuelekea Israel yalifanikiwa kupita katika mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel na kuharibu kambi zake za kijeshi.

Gazeti la Washington Post limeandika katika ripoti yake kwamba kutokana na uchambuzi wa picha za satelaiti za majibu ya makombora ya Iran kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na athari zake, takriban makombora 22 ya masafa marefu ya Iran yalirushwa katika Kambi ya Nevatim Air, kusini mwa Jangwa la Negev na makombora matatu kwenye kituo cha Tel Nof.

Ripoti ya gazeti la Washington Post inaongeza kuwa: Kuna video nyingine zinazoonyesha angalau vichwa 2 vya makombora ya Iran vilitua karibu na makao makuu ya Shirika la Ujasusi na Operesheni Maalum la Israel (Mossad) na mashimo 2 makubwa yanaonekana kutokana na athari zake.

 

Aidha gazeti la Washington Post linasema katika ripoti yake hiyo kwamba, maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) na jeshi la Israel wamekataa kuzungumzia ripoti ya gazeti hili.

Juumanne iliyopita, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) lilitekeleza Operesheni Ahadi ya Kweli -2 kwa kuvuruumisha makombora mengi ambayo yalilenga vituo kadhaa vya anga, kambi za kijeshi na rada, pamoja na vituo vya njama na mipango ya mauaji dhidi ya viongozi wa Muqawama na makamanda wa SEPAH.