Iran: Marekani itashindwa kumuokoa Netanyahu na kipigo kijacho cha ‘kupoozesha’
-
Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi
Mkuu wa Majeshi ya Iran Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi ameapa kuwa vikosi vya ulinzi vitatoa jibu la “mapigo ya kupoozesha” kwa uchokozi mwingine wowote mpya wa kijeshi utakaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel; na akaonya kwamba, mapigo hayo yatakuwa makali kiasi cha kuifanya hata Marekani ishindwe kumuokoa Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo bandia aliyeamuru kuanzishwa vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Akihutubia hafla iliyofanyika mjini Tehran, Jenerali Mousavi amesema, Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa imeandaa jibu hilo dhidi ya uchokozi uliofanywa na utawala haramu wa Israel kwa kufuata agizo lililotolewa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
“Hata hivyo haikupatikana fursa ya kulitekeleza”, ameeleza kamanda huyo huku akisisitiza kuwa bila shaka yoyote taifa la Iran litatoa jibu hilo endapo Israel itafanya uchokozi mwingine.
“Kama wataishambulia tena Iran, wataona tunayoweza kuyafanya. Katika hali hiyo, hata Marekani yamkini itashindwa kumuokoa Netanyahu”.
Katika vita vya kulazimishwa vya Siku 12 vilivyoanzishwa Juni 13 dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulimwengu ulishuhudia uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na utawala wa kijinai wa Israel huku ukipewa msukumo na uungaji mkono mkubwa wa kijeshi na Marekani.
Hata hivyo, katika jibu na mapigo makali yaliyofuata mara baada ya uvamizi huo, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilifanya mashambulizi yaliyolenga shabaha kwa umakini wa kiwango cha juu na kuviteketeza vituo muhimu vya nyuklia, vya kijeshi na vya miundomsingi ya viwanda ya utawala dhalimu wa Kizayuni.
Mashambulio dhidi ya utawala huo haramu, yaliyojumuisha mamia ya makombora ya balestiki yakiwemo yabebayo vichwa kadhaa vya mabomu na ya hypersonic yalifanyika kupitia operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la Ahadi ya Kweli III…/