Makamanda wa juu waahidi kutoa kipigo kikali zaidi iwapo Iran itashambuliwa tena
Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Iran amewaonya maadui kwamba watapata kipigo kikali zaidi iwapo wataanzisha uchokozi mpya dhidi ya Iran.
Mousavi alitamka haya jana katika mkutano na waandishi wa habari pambizoni mwa shughuli ya kuwaenzi mashahidi wa vita vya karibuni vya siku 12 vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Iran.
Utawala wa Kizayuni uliishambulia Iran katika kitendo cha uchokozi tarehe 13 mwezi Juni na kuwaua shahidi maafisa wakuu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na mamia ya raia katika mashambulizi yaliyolenga makazi ya raia.
Juni 22 mwaka huu Marekani ilijiunga katika vita hivyo kwa kuvishambulia vituo vikuu vitatu vya nyuklia vya Iran; ambapo Iran pia ilijibu kwa nguvu hujuma hiyo dhidi yake kwa kuvurumisha droni na makombora ya balistiki katika maeneo kadhaa muhimu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kusababisha maafa na uharibifu mkubwa.
Juni 24 pia yaani masaa kadhaa kabla ya kuanza kutekelezwa usitishaji vita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliipiga kwa makombora kambi kuu ya kijeshi ya Marekani huko Qatar ikiwa ni katika kujibu mashambulizi dhidi ya vituo vyake vya nyuklia.
Marasimu ya jana Jumatano yalifanywa siku nne baada ya kufanyika mazishi makubwa katika mji mkuu wa Iran, Tehran kwa ajili ya kutoa heshima na kuwaaga maafisa wa jeshi na wanasayansi watajika pamoja na makumi ya raia wa Iran waliouawa shahidi katika mashambulizi ya Israel. Rais Masoud Pezeshkian na viongozi wengine wa serikali na jeshi pia walishiriki katika marasimu hayo katika Msikiti Mkuu wa Mosalla hapa mjini Tehran.