Rais Pezeshkian: Taifa la Iran limetoa somo kubwa kwa wavamizi wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127934-rais_pezeshkian_taifa_la_iran_limetoa_somo_kubwa_kwa_wavamizi_wa_kizayuni
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amelaani hujuma ya hivi majuzi ya Israel dhidi ya Iran, na kusisitiza kwamba jeshi la Iran limetoa jibu madhubuti ambalo lilizuia kuenea kwa vita na kulinda mamlaka ya taifa.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jul 04, 2025 11:58 UTC
  • Rais Pezeshkian: Taifa la Iran limetoa somo kubwa kwa wavamizi wa Kizayuni

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amelaani hujuma ya hivi majuzi ya Israel dhidi ya Iran, na kusisitiza kwamba jeshi la Iran limetoa jibu madhubuti ambalo lilizuia kuenea kwa vita na kulinda mamlaka ya taifa.

Akizungumza mapema leo katika Mkutano wa 17 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) katika mji wa Khankendi nchini Azerbaijan, Rais Pezeshkian amelaani vitendo vya kihalifu vya Israel, ambavyo vililenga vikosi vya jeshi, maprofesa wa vyuo vikuu, raia wa kawaida, vituo vya amani vya nyuklia vilivyo chini ya uangalizi wa kimataifa, na miundombinu ya umma.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameyataja mashambulio ya siku 12 ya Israel, ikisaidiwa na Marekani, kuwa ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Kifungu cha 2, Ibara ya 4, ambacho kinakataza matumizi ya nguvu dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya nchi huru.

Rais Pezeshkian ameashiria uhalifu uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita hivyo dhidi ya taifa la Iran na kusema: Kwa mujibu wa Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, jeshi la Iran lilichukua hatua ya kulinda taifa, mamlaka ya kujitawala na ardhi ya nchi yetu, na kutoa somo kubwa kwa wavamizi na hivyo kuzuia kuenea kwa vita katika eneo la Magharibi mwa Asia." 

Mkutano wa 17 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi, ECO

Vilevile amezipongeza nchi wanachama wa ECO na nchi za kikanda kwa uungaji mkono wao na kulaani uchokozi wa Israel, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika kukabiliana na vitisho kutoka nje.

"Jumuiya nyingi za kikanda na kimataifa, ukiwemo Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Kiislamu, zimelaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesema Rais Pezeshkian.

Ameongeza kuwa: "Mkutano wa 17 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi pia ni fursa muhimu ya kumulika tena uchokozi wa hivi karibuni - na vitisho vyake vya kikanda na kimataifa."