Iran yanakusha madai ya kuvuruga usalama katika Bahari Nyekundu
(last modified Mon, 07 Oct 2024 02:21:27 GMT )
Oct 07, 2024 02:21 UTC
  • Iran yanakusha madai ya kuvuruga usalama katika Bahari Nyekundu

Mwakilishi wa Iran katika Kamati ya Ulinzi wa Mazingira ya Baharini (MEPC) amekadhibisha madai yaliyotolewa na Marekani dhidi ya Iran kuhusu usalama wa Bahari Nyekundu.

Pouria Kolivand amesema Iran ni mwaminifu kwa ahadi zake zote, na kusistiza kwamba Marekani ndiyo imesababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo hasa katika maji ya Bahari Nyekundu, kupitia kuunga mkono utawala wa Israel.

Kolivand alisema hayo katika kikao cha 82 cha Kamati ya Ulinzi wa Mazingira ya Baharini MEPC kilichofanyika London. Wakati wa kikao hicho, nchi chache zikiongozwa na Marekani zilitoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran.

Taarifa ya malalamiko ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ilisomwa katika kikao hicho kuhusu kuchelewa kutolewa kwa viza za ujumbe wa Iran na serikali ya Uingereza.

Haya yanajiri siku chache baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Ansarullahi ya Yemen kusema kuwa, imefanikiwa kuwatimua wanajeshi wa Marekani katika Bahari Nyekundu.

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimefunga njia zote za Bahari Nyekundu kuzuia vyombo vya Israel, Marekani na kila chombo cha baharini kisipeleke chochote kwa utawala wa Kizayuni, hatua ambayo inaendelea kuisababishia hasara kubwa Israel.

Tags