Ufaransa yaondoka katika kituo kingine cha kijeshi Senegal
Ufaransa imekabidhi kituo cha mawasiliano ya kijeshi kilichoko magharibi mwa Senegal kwa serokali ya nchi hiyo baada ya kuondoa wanajeshi wake. Rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi, Bassirou Diomaye Faye, mwaka jana alitaka kusitishwa kwa mkataba wa ulinzi uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya Senegal na mkoloni wa zamani, akisema mkataba huo “hauendani” na uhuru wa taifa lake.
Kituo hicho kilichopo Rufisque, kimekuwa kikihusika na mawasiliano ya kijeshi katika pwani ya kusini ya Atlantiki tangu mwaka 1960, kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi wa Ufaransa mjini Dakar, mji mkuu wa Senegal.
Paris ilianza kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Senegal mwezi Machi, ambapo vituo vya kijeshi vya Marechal na Saint-Exupery vilikabidhiwa kwa serikali ya Senegal. Mnamo Mei, Wafaransa waliondoka katika kambi ya Contre-Amiral Protet iliyopo bandarini Dakar. Tume ya pamoja iliyoanzishwa na mataifa hayo mawili ili kusimamia mchakato huo ilisema kuwa makabidhiano ya vituo na kuondoka kwa takribani wanajeshi wa Kifaransa 350 yatahitimishwa kufikia mwisho wa mwaka huu.
Hata hivyo, ubalozi wa Ufaransa ulisema Jumanne kuwa “maeneo ya mwisho yatakabidhiwa kufikia mwisho wa Julai 2025, kwa mujibu wa ratiba iliyokubaliwa kwa pamoja.
Senegal ilijipatia uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960 na kwa muda mrefu imekuwa mshirika wa serikali ya Ufaransa katika eneo la Afrika Magharibi. Hata hivyo, mwezi Novemba mwaka jana, Rais Bassirou Diomaye Faye, aliyeingia madarakani Aprili 2024, alitangaza uamuzi wake wa kuliondoa kabisa jeshi la Ufaransa nchini humo.
Mapema mwaka huu, Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko alisema kuwa Ufaransa haina uwezo wala uhalali wa kuhakikisha usalama na uhuru wa Afrika. Kauli yake ilikuja baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kudai kuwa mataifa ya eneo la Sahel “yamesahau” kuishukuru Paris kwa kuingilia kijeshi dhidi ya vitisho vya kigaidi, kauli iliyozua hasira kubwa barani Afrika.
Wanajeshi wa Kifaransa wamefukuzwa Mali, Burkina Faso, na Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hizo tatu za Sahel. Chad pia ilisitisha makubaliano yake ya ushirikiano wa ulinzi na Ufaransa mwaka jana. Mnamo Februari, Ufaransa ilikabidhi kambi yake ya kijeshi ya Port-Bouet – iliyokuwa ya pekee nchini Côte d’Ivoire (Ivory Coast) – kwa mamlaka za taifa hilo la Afrika Magharibi. Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alisema katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka mwezi Desemba kuwa kuondoka kwa takribani wanajeshi wa Kifaransa 600 kunalenga kuboresha majeshi ya taifa hilo.