Rais wa Iran aidhinisha kusitisha ushirikiano na IAEA kufuatia azimio la kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127858-rais_wa_iran_aidhinisha_kusitisha_ushirikiano_na_iaea_kufuatia_azimio_la_kisiasa
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, ameidhinisha rasmi sheria ya kusitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kufuatia azimio la kisiasa lililochochea hatua za uchokozi kutoka Marekani na Israel dhidi ya Iran.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jul 02, 2025 08:24 UTC
  • Rais wa Iran aidhinisha kusitisha ushirikiano na IAEA kufuatia azimio la kisiasa

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, ameidhinisha rasmi sheria ya kusitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kufuatia azimio la kisiasa lililochochea hatua za uchokozi kutoka Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Leo Jumatano, Pezeshkian ametangaza rasmi sheria hiyo inayotaka serikali ya Iran kusitisha ushirikiano wake na IAEA, baada ya kuidhinishwa na Bunge la Iran katika kikao chake cha hadhara tarehe 25 Juni.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wakaguzi wa IAEA hawataruhusiwa kuingia nchini Iran hadi usalama wa maeneo ya nyuklia na shughuli zake za nyuklia kwa matumizi ya amani zitakapohakikishwa, jambo ambalo litahitaji idhini ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.

Iran pia inazingatia kumpiga marufuku kuingia nchini Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, ambaye amekosolewa vikali kwa ripoti zake ambazo ni za kibaguzi na kisiasa dhidi ya Iran.

Bodi ya Magavana ya IAEA ilitumia ripoti ya Grossi katika kikao chake cha hivi karibuni kupitisha azimio dhidi ya Iran, ambalo lilitumiwa na utawala wa Israel kama kisingizio cha kushambulia Jamhuri ya Kiislamu.

Katika shambulizi la kichokozi mnamo Juni 13, Israel iliwalenga makamanda wa kijeshi wa Iran na wanasayansi wa nyuklia waliokuwa tayari wamewekwa kwenye orodha ya vikwazo kutokana na ripoti za IAEA. Rai wa kawaida, wakiwemo wanawake na watoto pia waliuawa katika mashambulizi hayo ya Israel.

Mnamo Juni 22, Marekani ilishambulia maeneo ya nyuklia ya Natanz, Fordow na Isfahan, jambo linalokiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Grossi amekataa kulaani mashambulizi hayo, hali iliyowakera viongozi wa Iran.

Katika barua aliyomwandikia Grossi, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), Mohammad Eslami, alieleza masikitiko yake juu ya kimya cha IAEA kuhusu uchokozi wa Israel dhidi ya Iran, likiwemo shambulizi la moja kwa moja dhidi ya vituo vyake vya nyuklia.