Oct 07, 2024 11:02 UTC
  • SEPAH: Tumejiandaa kikamilifu kukabiliana na jinai yoyote ya adui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa jeshi hilo linajivunia nishani ya Fat'h ambayo Amirijeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amemtunuku Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba jeshi hilo imara la Iran limejiandaa kikamilifu kupambana na jinai yoyote ile ya adui.

Jana Jumapili, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran alimtunuku nishani ya Fat'h, Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kutokana na kazi kubwa aliyoifanya hasa ya kuendesha kwa mafanikio ya kupigiwa mfano; Operesheni ya Ahadi ya Kweli II iliyoitia adabu Israel.

Nishani ya Fat'h imeanzishwa kama nembo ya operesheni za ushindi za wanamuqawama wa Kiislamu na mashujaa wa operesheni hizo. Nishani hiyo inajumuisha majani matatu ya mitende, kuba la Msikiti Mkuu wa Khorramshahr na bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran akimtunuku nishani ya Fat'h, Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH  amemtumia barua ya pongezi, Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga na Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kumtunuku nishani muhimu ya Fat'h kutokana na mafanikio makubwa aliyopata katika kulitumikia taifa na Uislamu.

Sehemu moja ya barua hiyo imesema: Kutunukiwa kwako "Nishani ya Fat'h" baada ya kuendesha kwa mafanikio Operesheni ya Ahadi ya Kweli II ambayo imefanyika kwa mafanikio na kuutia adabu utawala wa kigaidi wa Kizayuni unaomwaga damu za watu wasio na hatia, kumenifurahisha mimi na jeshi zima la SEPAH na tunajivunia nishani hiyo. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limejiandaa kikamilifu kukabiliana na jinai yoyote ya adui."