Oct 07, 2024 02:20 UTC
  • Jenerali Naqdi: Tutaishtaki US kwa kupuuza Mkataba wa Algiers

Naibu Kamanda wa Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC anayesimamia masuala ya uratibu amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itafungua kesi dhidi ya Marekani mwezi ujao kwa kushindwa kwake kutekeleza Mkataba wa Algiers kuhusiana na kurejeshwa mali za Iran.

Jenerali Mohammad Reza Naqdi alisema hayo jana Jumapili na kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajiandaa kuishtaki Marekani mnamo Novemba 3 kutokana na kushindwa kutekeleza Mkataba wa Algiers wa kurejesha hapa nchini mali za Iran.

Mkataba wa Algiers uliweka bayana kwamba, Washington inapaswa kurejesha milki zilizoporwa za Iran, ambazo zilihamishiwa Marekani na utawala wa Shah. Hata hivyo, kwa mujibu wa Jenerali Naqdi, Marekani mpaka sasa haijatimiza ahadi yake.

Kwingineko katika matamshi yake, Jenerali Naqdi ameashiria jinai za utawala wa Kizayuni unaofanywa huko Gaza na kubainisha kwamba, mashirika ya Marekani yametenga zaidi ya dola bilioni 300 kwa ajili ya kuunga mkono utawala wa Kizayuni.

Amebainisha kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utalazimika kukabiliana na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS peke yake, hautasalimika na kusisitiza kuwa, Muqawama ndio mshindi katika mzozo huo.

Aidha Naibu Kamanda wa IRGC anayesimamia masuala ya uratibu ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni unapigania maslahi ya Marekani huku akionya kuwa, Marekani ndiyo itakayoshindwa katika vita vya eneo hili, kwani imefungamanisha hatima yake na utawala huo bandia.

Tags