Araghchi: Iran ni muathiriwa mkuu wa silaha za kemikali hivyo inazipinga
(last modified Mon, 30 Jun 2025 11:08:38 GMT )
Jun 30, 2025 11:08 UTC
  • Araghchi: Iran ni muathiriwa mkuu wa silaha za kemikali hivyo inazipinga

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama taifa lililoathirika zaidi na silaha za kemikali katika historia ya sasa, ni mtetezi imara wa dunia isiyo na silaha za maangamizi.

Araghchi alitoa kauli hiyo katika ujumbe wake Jumapili, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Silaha za Kemikali na Biolojia, ambayo huadhimishwa kila mwaka wakati wa kumbukumbu ya shambulizi la kemikali dhidi ya mji wa Sardasht kaskazini-magharibi mwa Iran, lililotekelezwa na dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam, miaka 38 iliyopita.

Aragchi amesema: “Iran, ikiwa mwanzilishi mkuu wa wazo la eneo huru lisilo na silaha za nyuklia, imekuwa mstari wa mbele katika kupinga silaha hizi.”  Ameongeza kuwa Iran haijawahi kusitisha harakati zake za kutafuta haki kwa waathirika wa vita vya kemikali, na inaamini kuwa utekelezaji wa haki ni “sharti la msingi” katika kuzuia kurudiwa kwa uhalifu kama ule wa Sardasht.

Mnamo Juni 28, 1987, utawala wa Saddam ulirusha mabomu ya gesi ya haradali (mustard gas) katika mji wa Sardasht, na kuwaua takribani raia 119 wa Iran na kuwajeruhi wengine 8,000, wakiwemo waliobaki na ulemavu wa kudumu.

Araghchi amesema nchi za Magharibi — zikiwemo Ujerumani, Uholanzi, Uingereza, Ufaransa, na Marekani — zilitumia usaidizi wao wa kiteknolojia na vifaa katika kuchochea na kufanikisha mpango wa silaha za kemikali wa Iraq wakati huo. “Ushahidi wa kuaminika na nyaraka zilizothibitishwa zinaonyesha wazi kuwa nchi hizo, hasa Marekani, Uingereza, na Ujerumani, ziliipatia Iraq vifaa, teknolojia, na kemikali zilizotumika dhidi ya watu wa Iran,” amesisitiza.

Araghchi pia amegusia mauaji yanayoendelea ya raia wa kawaida wa Iran, wanawake, watoto, maprofesa wa vyuo vikuu, wanasayansi wa nyuklia, pamoja na maafisa waandamizi wa kiraia na kijeshi, akisema kwamba yote haya yanatekelezwa na magaidi wa kisasa na waovu walioko Tel Aviv.

“Nchi zile zile za Magharibi zimejiunga na mnyanyasaji, zikiendelea kutoa msaada wa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa vitendo vya uchokozi na ukiukaji wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa,” ameongeza kwa msisitizo.

Katika hitimisho la ujumbe wake, Waziri Araghchi amesifu uvumilivu, mshikamano, umoja na ujasiri wa taifa la Iran katika kukabiliana na uchokozi wa karibuni wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani, akisema kwamba wananchi wa Iran wameendelea kusimama imara dhidi ya dhulma, licha ya mateso.