Jenerali Mkuu: Iran inatilia shaka kufungamana Israel na usitishaji vita
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Iran, Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu dhamira ya Israel kutekeleza usitishaji mapigano wa upande mmoja uliotangazwa na Marekani, na akaonya kuwa Iran iko tayari kujibu kwa nguvu kubwa iwapo utawala huo utarejelea uchokozi wake.
Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Khalid bin Salman, yaliyofanyika Jumapili, Meja Jenerali Mousavi alisema Iran haikuchochea vita, bali ilijibu uchokozi kwa uwezo mkubwa.
Ameongeza kuwa: “Sisi hatukuanzisha vita, bali tulijibu kwa nguvu dhidi ya mchokozi. Na kwa kuwa tuna shaka ya kweli kuhusu kufungamana adui na ahadi zake, ikiwemo ya usitishaji mapigano , tupo tayari kujibu kwa kishindo iwapo watarudia uchokozi wao."
Katika mazungumzo hayo, walijadili vita vya siku 12 vya Israel na Marekani dhidi ya Iran, pamoja na masuala ya kikanda na mahusiano ya pande mbili.
Israel ilisimamisha mashambulizi yake dhidi ya Iran Jumanne iliyopita kwa upande mmoja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza usitishaji mapigano. Kwa mujibu wa mshauri wake wa zamani, Steve Bannon, Tel Aviv ililazimika kukubali ili “kujiokoa” kutokana na kiwango cha mashambulizi waliyoyaanzisha kuzidi uwezo wao wa kivita.
Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumatano, Bannon alisema kuwa usitishaji mapigano uliopatanishwa na Trump kwa msaada wa Qatar, “ulikuwa njia ya kuilinda Israel.”
Mashambulizi hayo ya Israel yalianza tarehe 13 Juni, yakilenga makamanda wa juu wa kijeshi wa Iran, wanasayansi wa nyuklia, pamoja na raia wa kawaida, wakiwemo wanawake na watoto.
Katika kujibu, vikosi vya ulinzi vya Iran viliishambulia kwa makombora ya hali ya juu, ambayo yalivunja mifumo ya ulinzi ya Israel iliyokuwa ikihesabiwa kuwa na uwezo mkubwa.
Jeshi la Iran lilishambulia miundombinu ya kijeshi na viwanda ya utawala wa Kizayuni kwa kutumia makombora ambayo yalipiga malengo yaliyolengwa kwa ufanisi mkubwa.
Jenerali Mousavi amesema kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni zimeonesha kuwa hazizngatii sheria wala kanuni zozote za kimataifa, jambo ambalo dunia ililishuhudia katika vita hivi vya siku 12 vilivyoanzishwa kwa mabavu.
Kwa upande wake, Mwanamfalme Khalid amesema kuwa serikali ya Saudi Arabia haikutosheka tu kwa kulaani uchokozi huo, bali ilifanya juhudi kubwa kumaliza vita hivyo na mashambulizi dhidi ya Iran.
Aliwasilisha pia salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali ya Saudi Arabia kwa kuuawa shahidi kwa makamanda wa Iran wakati wa mashambulizi ya kichokozi ya Israel.
Pande zote mbili zilikubaliana kuendeleza mashauriano ili kuimarisha mahusiano ya pande mbili, kudumisha usalama na amani ya kikanda, na kubainisha nafasi muhimu ya Iran na Saudi Arabia katika kufanikisha malengo hayo.