Larijani: Israel ilipanga lakini ilishindwa kumuua Kiongozi Muadhamu wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127780-larijani_israel_ilipanga_lakini_ilishindwa_kumuua_kiongozi_muadhamu_wa_iran
Mshauri wa ngazi ya juu wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, amefichua kuwa Israel ilikuwa imepanga kushambulia mkutano wa ngazi ya juu wa maafisa wa Iran—wakiwemo viongozi wa serikali—na baadaye kumlenga Kiongozi Muadhamu mwenyewe, lakini mpango huo ulizimwa kwa mafanikio.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jun 30, 2025 07:32 UTC
  • Ali Larijani
    Ali Larijani

Mshauri wa ngazi ya juu wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, amefichua kuwa Israel ilikuwa imepanga kushambulia mkutano wa ngazi ya juu wa maafisa wa Iran—wakiwemo viongozi wa serikali—na baadaye kumlenga Kiongozi Muadhamu mwenyewe, lakini mpango huo ulizimwa kwa mafanikio.

Akizungumza Jumapili katika mahojiano ya televisheni, Larijani aliongeza kuwa:  “Mipango ya adui katika vita hii ilikuwa kuwalenga makamanda wa IRGC na vituo muhimu vya kitaifa kwa wakati mmoja. Walidhani wangeweza kuwashinikiza baadhi ya viongozi wa serikali kuusaliti mfumo wa Kiislamu kwa vitisho.”

Larijani, aliyekuwa Spika wa Bunge kati ya 2008 na 2020, alifichua zaidi kuwa wakati wa vita, Israel ilijaribu kutisha maafisa mbalimbali wa Iran, ikiwa ni pamoja na wanasiasa, maafisa wa kijeshi na maafisa wa usalama.

Akifafanua zaidi alisema: “Ijumaa walinipigia simu na kunipa saa 12 kuondoka Iran au kutoka Tehran, la sivyo ningepitia hatima kama ya mashahidi kama Jenerali Mkuu wa Majeshi ya Iran, Mohammad Hossein Bagheri na kamanda wa ngazi za juu wa kijeshi, Jenerali Mkuu Gholam-Ali Rashid. Niliwapa jibu walilostahili."

Akirejelea mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya amani ya nyuklia ya Iran kama Fordow, Natanz na Isfahan, Larijani alifafanua kuwa ni “juhudi za kuokoa sura,” na kusema, “ acha waendelee kufurahia hilo.”

Akitaja hatua za Iran za kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Marekani nchini Iran, Larijani alisema, “kati ya makombora 14 ya Iran, 6 yalilenga kambi ya Marekani nchini Qatar - na yalipiga kwa nguvu, kila moja likiwa na kilo 400 za mada za milipuko.”

Larijani amesema Rais Donald Trump wa Marekani, alijaribu kuokoa sura, kwa kudai kuwa ni  'kombora moja tu ndilo lililopiga kambi hiyo,' kwa hivyo tunamruhusu “afurahie ndoto zake.”