Iran yasema inafuatilia kwa karibu harakati zozote za Israel katika nchi jirani
(last modified Mon, 30 Jun 2025 11:16:46 GMT )
Jun 30, 2025 11:16 UTC
  • Iran yasema inafuatilia kwa karibu harakati zozote za Israel katika nchi jirani

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa inafuatilia kwa karibu hatua zozote za utawala wa Kizayuni wa Israel zinazolenga kutumia ardhi ya nchi jirani kwa ajili ya vitendo vya uchokozi dhidi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wake wa kila wiki siku ya Jumatatu, Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema kuwa Tehran tayari imezieleza nchi husika kuhusu taarifa, habari za kiintelijensia, na uvumi unaohusiana na suala hilo.

Baghaei amesema: “Bila ubaguzi wowote, nchi zote jirani zimetuhakikishia kuwa hazitaruhusu kabisa utawala wa Kizayuni kutumia anga au ardhi yao kwa mashambulizi dhidi ya Iran.”

Ameongeza kuwa nchi hizo zinafahamu kikamilifu wajibu wao, kwa mujibu wa sera ya ujirani mwema na sheria za kimataifa.

Amesema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hakuna taifa linaloruhusiwa kuruhusu taifa jingine kutumia ardhi yake kwa vitendo vya uhasama dhidi ya nchi ya tatu.

Baghaei amefafanua kuwa nchi husika zimekanusha waziwazi taarifa zinazoeleza kuwa ardhi yao inatumiwa au itatumiwa dhidi ya Iran, na zimetoa dhamana kwamba hazitakubali jambo hilo kutokea hata katika siku zijazo.

Amesisitiza kuwa uchunguzi juu ya suala hili bado unaendelea, huku jeshi la Iran pamoja na vyombo vya usalama na kijeshi vikiendelea kulifuatilia kwa makini. Vilevile, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inaendelea kulifuatilia kwa umakini mkubwa.

Kuhusu taarifa ya hivi karibuni ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA), Baghaei amesema ripoti hiyo “isiyofaa” imekuwa kisingizio kwa Marekani na Israel kufanya uchokozi wa kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Amesema: “Marekani na mataifa matatu ya Ulaya – Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani – pamoja na nchi nyingine, zimechukua mtazamo wa kisiasa dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran."

Amekosoa IAEA kwa makosa yake yaliyoibua matatizo katika suala la nyuklia la Iran na hivyo kuyafanya mazungumzo ya ushirikiano yasiwe na maana tena.

Amehitimisha kwa kusema: “Tunatarajia wakati huu kuwa wakala huu na mkurugenzi wake mkuu watafanya kazi kwa mujibu wa wajibu wao wa kitaalamu, bila kujihusisha na mbinu za kisiasa."