Kiongozi wa upinzani anayezuiliwa Chad akomesha mgomo wa kula
Kiongozi wa upinzani nchini Chad aliyewahi kuwa waziri mkuu, Succes Masra, amekomesha mgomo wa kula baada ya takriban wiki moja.
Hayo yametangazwa na mawakili wake katika taarifa iliyotolewa na chama chake jana Jumatatu.
Masra alitangaza mgomo wa kula wiki iliyopita kupinga kuzuiliwa kwake katika mji mkuu, N'Djamena.
Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani cha Chad Les Transformateurs (The Transformers) na waziri mkuu wa zamani, alikamatwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Mei 16 kufuatia ghasia zilizotokea katika jimbo la Logone Occidental na kusababisha vifo vya watu 42 mnamo Mei 14.
Masra ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi, kuanzisha uasi, kushirikiana na makundi yenye silaha na kupanga njama za mauaji, tuhuma ambazo zote amezikanusha.
Succes Masra aligombea katika uchaguzi wa urais wa Mei 2024, ambao ulimpa ushindi rais wa mpito wa wakati huo, Mahamat Idriss Deby.
Mwezi uliopita, Human Rights Watch ilitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Masra "ikiwa hatashtakiwa kwa kosa halali."