Baqaei: Iran inataka amani lakini haitasalimu amri mbele ya ukandamizaji
Esmaile Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Iran imejidhatiti kwa ajili ya suala la amani, lakini kwamba haitasalimu amri abadan mbele ya maadui
Iran imejitolea kudumisha amani, lakini kamwe haitakubali udhalilishaji au uchokozi wowote dhidi yake.
Baqaei ameeleza haya leo katika shughuli ya kuwaaga wananchi wa Iran waliouawa shahidi katika mashambulizi ya kijeshi ya Israel hivi karibuni; siku ambayo imesadifiana na tarehe pili Muharram.
Maombolezo ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) yanafanyika katika siku kumi za mwanzo za mwezi wa Muharram katika hali maalumu kote nchini Iran. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika mahojiano yake na televisheni ya Press amedokeza kuhusu imani ya wananchi wa Iran kwa siku ya Ashura.
Amesema, wananchi wa Iran wakiongozwa na thamani za kiutu na kujitolea siku zoke wameonyesha istiqama na kusimama imara mbele ya vitisho dhidi yao.
"Umati mkubwa wa waombolezaji uliojitokeza leo Tehran katika shughuli ya maziko umedhihirisha fakhari ya taifa na mshikamano", amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Shughuli ya mazishi ya Wairani waliopoteza maisha katika mashambulizi ya Israel dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefanyika katika mji mkuu Tehran, kwa kuhudhuriwa na Rais Masoud Pezeshkian, Mohammad Baqer Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), Waziri wa Mambo ya Nje Sayyid Abbas Araqchi na maafisa wengine kadhaa wa ngazi za juu.