Oct 06, 2024 02:50 UTC
  • Ethiopian Airlines yasimamisha safari zote za ndege za kuelekea Israel

Shirika la Ndege la Ethiopia limetangaza kusitisha safari zote za ndege za kuelekea Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, hadi itakapotangazwa tena kutokana na hali ilivyo sasa katika eneo la Asia Magharibi.

Katika taarifa yake rasmi, Ethiopian Airlines imetangaza pia kusimamisha safari zake kuelekea Beirut, mji mkuu wa Lebanon. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo umekuja ikiwa ni sehemu ya jitihada za shirika hilo za kuthamini sana usalama wa abiria na kutekeleza maelekezo ya mamlaka husika.

Shirika hilo la ndege la Ethiopia limesema pia kuwa, linafuatilia kwa karibu matukio ya eneo hilo na linawasiliana na mamlaka husika.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: "Kama unapenda kuakhirisha safari, Ethiopian Airlines inakurejeshea pesa zako zote. Unaweza kuwasiliana na wakala wako wa usafiri au wasiliana na shirika la ndege moja kwa moja."

Shirika hilo la ndege la Ethiopia limeelezea kusikitishwa kwake na usumbufu uliosababishwa na hatua hiyo ya kusimamishwa safari za ndege, lakini limesisitiza kwamba, linaupa umuhimu mkubwa usalama wa abiria kwani ndicho kipaumbele chake cha kwanza.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya jinai za kutisha za kushambulia maeneo ya raia huko Palestina na Beirut, Lebanon. Lakini majibu yanayotolewa na wanamapambano wa Kiislamu dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni, yanaisababishia hasara kubwa Israel hasa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mashirika mengi ya ndege kusimamisha safari zao kuelekea maeneo ya utawala huo pandikizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.