Umuhimu wa kuwepo umoja na ushirikiano wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na muendelezo wa vita vya utawala wa Kizayuni
Uchokozi na vita vya utawala haramu wa Israel katika eneo vimeongeza maradufu, jambo linalotoa udharura wa kuwepo umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na utawala huo ghasibu.
Utambulisho na tabia ya kupenda vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel imevuruga zaidi hali ya usalama ya eneo hili kuliko wakati mwingine wowote, na hivyo kuongeza maradufu haja ya nchi za Kiislamu kushirikiana na kuwa na umoja kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo. Licha ya kushindwa kijeshi mtawalia huko Ukanda wa Gaza dhidi ya makundi ya muqawama wa Palestina, Wazayuni bado wanaendeleza vitendo vyao vya kinyama na kikatili katika eneo ambapo sasa wanapanga kueneza migogoro katika eneo, baada ya Gaza, Lebanon, Syria na hata Iraq.
Wazayuni wanaendeleza jinai zao huko Gaza na Lebanon katika hali ambayo Marekani na serikali za Magharibi ambazo ni waungaji mkono wakuu wa Tel Aviv zimenyamaza kimya, nao Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kushindwa kuchukua hatua yoyote ya maana ya kuuadhibu utawala huo kutokana na jinai unazofanya dhidi ya raia wasio na hatia. Kwa kuzingatia uungaji mkono huo wa nchi za Magharibi na kushindwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua, watawala watendajinai wa Tel Aviv wamemea pembe zaidi na kuamua kuendeleza jinai zao dhidi ya watu wa Lebanon na Gaza bila huruma.

Suala muhimu kuhusiana na hali hii ya kusikitisha ni kuwepo ushirikiano wa nchi za Kiislamu, jambo ambalo linaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuzima mashine ya mauaji ya kizazi ya Wazayuni. Dhamiri zenye mwamko leo katika Ulimwengu wa Kiislamu zimekataa kuketi kimya mbele ya jinai hizi za Wazayuni, ambapo kumedhihiri wimbi kubwa la uungaji mkono kwa wananchi madhlumu wa Palestina na Lebanon katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kinyume na matakwa ya utawala ghasibu wa Israel.
Ushirikiano wa viongozi wa Ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na hali ya eneo bila shaka unaweza kuwa a mchango mkubwa katika kuunda mrengo madhubuti wa kisiasa dhidi ya siasa haribifu za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Waislamu. Uungaji mkono mkubwa kwa wananchi wa Palestina na Lebanon na kutopuuza masaibu na hali ngumu wanayoipitia bila shaka kutaulazimisha utawala wa Kizayuni kusimamisha mauaji ya kimbari na kuwasukuma watawala watendajinai wa Tel Aviv na waungaji mkono wao wa Magharibi katika mahakama za kimataifa.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), ikiwa ni taasisi yenye taathira katika ulimwengu wa Kiislamu na yenye wanachama zaidi ya nchi 50, ina jukumu muhimu la kuhamasisha umoja na ushirikiano katika ulimwengu wa Kiislamu. Ni wazi kuwa taasisi hii inaweza kudhamini matakwa ya Waislamu duniani kuhusiana na suala zima la Palestina na kuuadhibu utawala haramu wa Israel.
Moja ya nukta muhimu kuhusu uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu, ni kutumiwa mbinu ya kiuchumi ili kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa Magharibi. Uwezo wa kiuchumi katika eneo hili ni mkubwa sana kiasi kwamba makampuni na taasisi nyingi kubwa za Magharibi haziwezi kumudu kuupuuza. Eneo la Asia Magharibi ndicho chanzo muhimu zaidi cha uzalishaji na usambazaji wa nishati kwa makampuni makubwa ya Marekani na Ulaya. Ulimwengu wa Kiislamu, katika vita vya nchi kadhaa za Kiarabu na utawala wa Kizayuni katika miaka ya 1970, kwa shabaha ya kukabiliana na Wazayuni, Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ulipiga marufuku uuzaji wa mafuta kwa makampuni makubwa ya nchi hizo, jambo ambalo lilikuwa na taathira kubwa katika uchumi wa nchi za Magharibi.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa jana tarehe 4 Oktoba, huku akifafanua miongozo ya Qur'ani Tukufu kuhusu suala la "mshikamano wa Kiislamu", alisisitiza kuwa: "Wilaya na utawala wa Waislamu unamaanisha kuwa umoja, huruma na ushirikiano huleta msaada wa heshima na busara kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mbapo matokeo yake huwa ni kuvuka vizuizi na kuwashinda maadui. Ameashiria siasa tofauti za kijeshi, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni zinazotekelezwa na maadui kwa ajili ya kuibua mifarakano miongoni mwa Waislamu na kusema: "Adui wa taifa la Iran ni yule yule adui wa mataifa ya Palestina, Lebanon, Misri, Syria, Iraq, Yemen na nchi nyingine za Kiislamu, na amri zote za kufanya hujuma na kibua migawanyiko hutoka kwenye chumba kimoja cha miongozo na maelekezo, na tofauti pekee ni mbinu tofauti zinazotekelezwa katika nchi tofauti za Kiislamu.
Jambo muhimu zaidi na la kimsingi ambalo linaweza kuongeza nguvu na uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu wa kukabiliana na utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wao wa Magharibi ni umoja na ushirikiano wa nchi hizo (Ulimwengu wa Kiislamu) kwa ajili ya kukabiliana na njama na malengo maovu ambayo Wamagharibi wanayafuatilia kwa kuibua migawanyiko na migogoro kati ya Waislamu.