Madaktari 99 wa US waliohudumu Ghaza: Hakuna ushahidi kama HAMAS imezitumia kijeshi Hospitali
(last modified Fri, 04 Oct 2024 09:40:30 GMT )
Oct 04, 2024 09:40 UTC
  • Madaktari 99 wa US waliohudumu Ghaza: Hakuna ushahidi kama HAMAS imezitumia kijeshi Hospitali

Kundi la madaktari 99 wa Kimarekani na wataalamu wa tiba waliojitolea kufanya kazi katika eneo lililozingirwa la Ukanda wa Ghaza wamesema hawakuona dalili zozote za kuwepo harakati za kijeshi zinazofanywa na kundi la Muqawama la Hamas katika hospitali za eneo hilo, na wameutaka utawala wa Joe Biden usitishe mara moja misaada na uungaji mkono wa kijeshi, kiuchumi na kidiplomasia kwa Israel.

Katika barua waliyomwandikia rais huyo wa Marekani na Makamu wake Kamala Harris, madakatari hao ambao kwa pamoja walitumia muda wa wiki 254 kuhudumu kwa kujitolea katika vituo vya afya vya Ghaza, wamesimulia tajiriba na uzoefu mchungu wa waliyojionea kwa macho yao kuhusu hali mbaya ya kibinadamu wakati wa mashambulizi ya kinyama yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel, wakisema "wameshuhudia uhalifu uzioweza kueleweka".
 
Sehemu moja ya barua hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti ya "Ghaza Healthcare Letters" imesema: "tunataka kuweka wazi kabisa: hakuna yeyote kati yetu aliyewahi kuona hata mara moja aina yoyote ya harakati za wanamgambo wa Kipalestina katika hospitali yoyote ya Ghaza au vituo vingine vya afya". 

Madaktari hao 99 wa Kimarekani wameendelea kubainisha katika barua yao kwa Biden wakisema: "tunakuhimizeni mulione hili, kwamba Israel imeharibu kwa mpangilio maalumu na kwa makusudi mfumo mzima wa huduma za afya wa Ghaza na kwamba Israel imewalenga wenzetu huko Ghaza kwa njia za mateso, utowekeshaji na mauaji".

 
Barua hiyo inaelezea pia mateso ya wanawake na watoto katika hospitali, ikiwa ni pamoja na kuenea kwa utapiamlo na ukosefu wa vifaa muhimu vya matibabu huko Ghaza.
 
Aidha, madaktari hao wameashiria utafiti uliochapishwa katika jarida la matibabu la Lancet mwezi Julai, ambao ulisema, athari za vita vya Israel dhidi ya Ghaza zinaweza kumaanisha kwamba idadi halisi ya vifo katika eneo hilo imepindukia watu 186,000.../