Watu 82 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa DAESH watiwa mbaroni Ethiopia
Shirika la Taifa la Intelijensia la Ethiopia limetangaza kuwa limewakamata watu 82 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).
Taarifa iliyotolewa Jumanne na shirika hilo imeeleza kwamba, watu hao waliokamatwa wanashukiwa kupewa mafunzo katika nchi jirani na kisha kuingia katika maeneo mbalimbali nchini Ethiopia.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, washukiwa hao wamekamatwa mjini Addis Ababa na katika kanda za Oromia, Amhara, Somali na Harari.
Mamlaka husika zimesema baadhi ya washukiwa waliokamatwa wanaaminika kuhusika katika vitendo vya uhalifu ikiwemo ukusanyaji wa taarifa za kijasusi, kutoa fedha na kuandaa mipango.
Shirika la Intelijensia la Ethiopia limebainisha kuwa, jamii za maeneo hayo zilisaidia kutoa taarifa zilizosaidia kuwakamata watu hao na kwamba uchunguzi unaendelea.../