Araghchi amjibu Trump: Vikosi vya Iran viko tayari kujibu mapigo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amemuonya Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu, akikosoa matamshi yake ya hivi karibuni na kuyaeleza kuwa "yasiyo na busara na hatarishi," na kusisitiza kwamba vikosi vya jeshi la Iran vimejiandaa kikamilifu kulinda mamlaka ya kujitawala nchi hii.
"Wale walioathiriwa na mabadiliko ya muda mfupi ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha za kigeni nchini Iran wamekuwa wakiandamana kwa amani hivi karibuni, na ni haki yao," Waziri wa Mambo ya Nje amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa na kusisitiza kuwa,"Tofauti na hilo, tumeshuhudia matukio machache ya ghasia za vurugu—ikiwa ni pamoja na mashambulizi kwenye kituo cha polisi na kuwarushia askari polisi mabomu ya kujitengenezea ya molotov."
Akirejelea rekodi ya ndani ya Trump, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema Rais wa Marekani anapaswa kuelewa kwamba vurugu dhidi ya mali za umma haziwezi kuvumiliwa popote.
Amesema, "Kwa kuzingatia kupelekwa kwa askari wa Gadi ya Taifa na Rais Trump ndani ya mipaka ya Marekani, yeye katika watu wote anapaswa kujua kwamba mashambulizi ya jinai dhidi ya mali za umma hayawezi kuvumiliwa."
Kabla ya hapo, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran alionya kwamba, uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu utavuruga utulivu wa eneo zima la Asia Magharibi na kuhatarisha moja kwa moja maslahi ya Marekani katika eneo.
Ali Larijani amesema hayo katika ujumbe alioutuma jana kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kwamba, misimamo ya hivi karibuni iliyochukuliwa na maafisa wa Israel na Rais wa Marekani, Donald Trump imeanika njama za nyuma ya pazia juu ya matukio ya sasa nchini.
Katika ujumbe kwenye jukwaa lake la Truth Social, Trump alibwabwaja kwamba: Ikiwa Iran "itawapiga risasi na kuwaua waandamanaji wa amani," Marekani "itakuja kuwaokoa."