Umoja wa Mataifa: Tuna wasiwasi kuhusu kuongezeka vurugu na machafuko Sudan Kusini
-
Umoja wa Mataifa: Tuna wasiwasi kuhusu kuongezeka vurugu na machafuko Sudan Kusini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa kwamba ana wasiwasi mkubwa kuhusu athari za kuongezeka vurugu na machafuko nchini Sudan Kusini, akiongeza kuwa hali hii itawadhuru zaidi raia ambao tayari wako katika hali hatarishi.
António Guterres amesisitiza hitajio la kuweka kipaumbele ulinzi wa raia na kuhakikisha utoaji salama wa misaada ya kibinadamu na usalama katika nchi ambapo theluthi mbili ya idadi ya watu inatarajiwa kuhitaji aina fulani ya usaidizi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akizunguumzia umuhimu wa kusitishwa shughuli za kijeshi, ametoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini na vikosi vya upinzani kuchukua "hatua za haraka na za uhakika za kusitisha shughuli zote za kijeshi na kupunguza mvutano kupitia mazungumzo jumuishi."
Licha ya mapigano makali kati ya vikosi vya jeshi la Sudan Kusini na vikosi vya upinzani katika siku za hivi karibuni, lakini serikali ya Sudan Kusini imesisitiza kwamba nchi hiyo haishiriki vitani.
Ateny Wek Ateny Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amewaambia waandishi wa habari mjini Juba kwamba "nchi hiyo haiko vitani, tunazuia tu kusonga mbele kwa vikosi vya upinzani."
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang, alitangaza Jumapili kwamba operesheni ya "Amani Endelevu" itaanza hivi karibuni, na jeshi limewaomba raia kuhama maeneo matatu katika jimbo la Jonglei.
Duru mpya ya mapigano nchini Sudan Kusini kati ya makundi yanayomtii Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu Riek Machar ilianza mwishoni mwa Desemba katika jimbo la Jonglei, kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.