Iran: IRGC inadumisha amani, utulivu; uingiliaji unachochea taharuki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136130-iran_irgc_inadumisha_amani_utulivu_uingiliaji_unachochea_taharuki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lina jukumu muhimu katika kudumisha amani na utulivu katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, huku akionya kwamba uwepo na vikosi vya kigeni katika eneo la Asia Magharibi umepelekea kuongezeka taharuki badala ya kupunguza mvutano.
(last modified 2026-02-01T07:01:20+00:00 )
Feb 01, 2026 07:01 UTC
  • Iran: IRGC inadumisha amani, utulivu; uingiliaji unachochea taharuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lina jukumu muhimu katika kudumisha amani na utulivu katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, huku akionya kwamba uwepo na vikosi vya kigeni katika eneo la Asia Magharibi umepelekea kuongezeka taharuki badala ya kupunguza mvutano.

Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa X jana Jumamosi, Araghchi amelinganisha umbali wa kijiografia wa Marekani kutoka eneo hilo na ukaribu wa Iran na Lango Bahari la Hormuz, akielezea harakati za kijeshi za Marekani zinazoendelea karibu na maji ya Iran kama jaribio la kuamrisha jinsi Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu vitakavyofanya luteka katika eneo na maji yao.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amekosoa misimamo ya kugongana ya Washington, akibainisha kuwa Kamandi Kuu ya Marekani CENTCOM ambayo imeiorodhesha IRGC kama "shirika la kigaidi," sasa inalizungumzia kama jeshi la kitaifa na kutoa maoni kuhusu maneva yake.

Araghchi alikuwa akiashiria hatua ya CENTCOM ya hivi karibuni, ikishauri kwamba IRGC izingatie "utaalamu" wakati wa mazoezi yao ya kijeshi katika Lango Bahari la Hormuz.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, matamshi hayo yaliashiria wazi hulka ya uingiliaji wa mara kwa mara wa Marekani katika masuala ya nchi nyingine, na wakati huo huo yalionyesha kutambuliwa rasmi IRGC kama jeshi linalolinda taifa huru.

"Hiki ndicho kiwango cha upuuzi ambacho dunia inakabiliwa nacho sasa hivi, na ambacho serikali za Ulaya zimeamua kukikumbatia kikamilifu," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza, akiashiria hatua ya Brussels ya hivi karibuni, ya kufuata kibubusa nyayo za Washington katika kuiweka IRGC kwenye orodha ya magaidi.