Maelfu waandamana kote Ulaya kuunga mkono Palestina, kulaani ukatili wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136142-maelfu_waandamana_kote_ulaya_kuunga_mkono_palestina_kulaani_ukatili_wa_israel
Waelfu kwa maelfu ya watu wamejitokeza mitaani katika nchi kadhaa za Ulaya kushiriki maandamano ya kuunga mkono Palestina, huku wakiushutumu utawala wa Israel kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza kati yake na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.
(last modified 2026-02-01T10:32:40+00:00 )
Feb 01, 2026 10:32 UTC
  • Maelfu waandamana kote Ulaya kuunga mkono Palestina, kulaani ukatili wa Israel

Waelfu kwa maelfu ya watu wamejitokeza mitaani katika nchi kadhaa za Ulaya kushiriki maandamano ya kuunga mkono Palestina, huku wakiushutumu utawala wa Israel kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza kati yake na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.

Makumi ya maelfu ya watu wameandamana katika majiji ya London na Stockholm Jumamosi wakiiunga mkono Palestina, na kupinga mashambulizi ya mauaji ya halaiki yanaloendeleza na wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, licha ya kusitishwa mapigano. Waandamanaji hao wametaka kusitishwa kwa mauzo ya silaha za Ulaya kwa utawala huo vamizi.

Umati mkubwa wa waandamanaji wanaounga mkono Palestina walikusanyika katika Uwanja wa Russell jijini London kabla ya kuandamana hadi Whitehall, yenye Ofisi ya Waziri Mkuu katika barabara ya 10 Downing Street na taasisi zingine za serikali kuu.

Maandamano hayo yalibeba jumbe za ndani na za kimataifa, huku waandamanaji wakiitaka serikali ya Uingereza isijiunge na kile kinachoitwa "Baraza la Amani," linaloonekana na waandamanaji kama jukwaa la kuikalia tena kwa mabavu Ukanda wa Gaza.

Nchini Sweden, mamia ya waandamanaji walikusanyika katika mji mkuu, Stockholm, kupinga mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na kuzuia misaada ya kibinadamu katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu. Maandamano hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Odenplan yameandaliwa na makundi kadhaa ya asasi za kiraia.

Mabango yaliyobebwa na waandamanaji yalisomeka: "Watoto wanauawa Gaza," "Shule na hospitali zinapigwa mabomu," "Komesha mashambulizi Gaza," "Komesha vikwazo vya chakula," na "Israel lazima izingatie makubaliano ya amani."

Haya yanajiri huku Wapalestina wasiopungua 31, wakiwemo kwa uchache watoto sita, wakiuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel tangu alfajiri ya jana katika Jiji la Gaza na mji wa Khan Younis katika Ukanda wa Gaza.

Vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel Oktoba 2023 dhidi ya Gaza vimewaua shahidi watu wasiopungua 71,769 na kuwajeruhi 171,483.