Wanaharakati waliotoweka Kenya katika maandamano ya Gen Z wapatikana wakiwa wameteswa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139494-wanaharakati_waliotoweka_kenya_katika_maandamano_ya_gen_z_wapatikana_wakiwa_wameteswa
Wanaharakati watano waliotoweka baada ya kukamatwa katika maandamano ya kumbukumbu ya Gen Z ya Juni 25, wamepatikana wakiwa na majeraha na sasa wanapewa matibabu katika Hospitali ya Nairobi Women’s.
(last modified 2026-06-28T14:10:41+00:00 )
Jun 28, 2026 14:07 UTC
  • Wanaharakati waliotoweka maandamano ya Gen Z wapatikana
    Wanaharakati waliotoweka maandamano ya Gen Z wapatikana

Wanaharakati watano waliotoweka baada ya kukamatwa katika maandamano ya kumbukumbu ya Gen Z ya Juni 25, wamepatikana wakiwa na majeraha na sasa wanapewa matibabu katika Hospitali ya Nairobi Women’s.

Wanaharakati hao wanadai walitekwa nyara, kuteswa na baadaye kutupwa maeneo tofauti jijini Nairobi.

Waliojitokeza ni Frederick Odhiambo Ojiro, Michael Ngige almaarufu Jomo Kenyatta Junior, Muteti Mulinge, Collins Ochieng na Elijah Alam.

Mwanaharakati mwingine, Davis Lichuma, hakuwa amepatikana kufikia alasiri ya jana Jumamosi, hali iliyozua hofu mpya kuhusu kutoweka watu kwa lazima.

Wanaharakati hao walidai walikamatwa karibu na Bunge wakati wa maandamano kabla ya kutoweka, jambo lililosababisha mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na waandamanaji kutaka polisi waeleze waliko.

Akizungumza akiwa hospitalini, Collins Ochieng amesema mara baada ya kukamatwa waliingizwa kwa nguvu ndani ya magari aina ya Subaru, wakafungwa vitambaa usoni na kupelekwa eneo lisilojulikana ambako waliteswa wakati wa kuhojiwa. Amedai waliokuwa wakiwahoji walitaka kujua ni nani anayefadhili maandamano hayo.

Ochieng amesema waliendelea kufungwa macho hadi saa saba usiku wa kuamkia jana Jumamosi walipoachiliwa na kutupwa kando ya Barabara ya Lang’ata.

Kwa upande wake, Frederick Odhiambo Ojiro amesema walipigwa vibaya wakiwa kizuizini na kwamba hata hawezi kutembea kutokana na majeraha aliyopata.

Matukio hayo yalijiri saa chache baada ya Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC) kutangaza kuwa watu sita waliokuwa wametoweka baada ya maandamano hayo wamepatikana katika maeneo tofauti ya Nairobi wakiwa na majeraha na kudai waliteswa wakiwa mikononi mwa waliowakamata.

Shirika la Amnesty International Kenya limetaka Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) pamoja na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu madai ya mateso na kutoweka kwa lazima.

Itakumbukwa kuwa, Polisi nchini Kenya Alkhamisi wiki hii walitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji katika maeneo mbalimbali mjini Nairobi huku makundi yanayoongozwa na vijana yakiadhimisha kumbukumbu ya miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi dhidi ya makumi ya vijana na wanaharakati waliokuwa wakitaka kuelekea kwenye majengo ya Bunge la Taifa kuweka mashada ya maua kuwakumbuka vijana waliouawa Juni 25, 2024 katika maandamano ya kupinga Mswada tata wa Fedha, ambayo yaliyogeuka kuwa machafuko ya kitaifa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 120, kulingakwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu.