Ruto asema serikali imetekeleza ahadi ilizowapa Waislamu wa Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140442-ruto_asema_serikali_imetekeleza_ahadi_ilizowapa_waislamu_wa_kenya
Rais William Ruto wa Kenya amesema serikali imetekeleza ahadi muhimu ilizotoa kwa jamii ya Waislamu wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2022.
(last modified 2026-08-06T03:31:30+00:00 )
Aug 06, 2026 03:24 UTC
  • Rais William Ruto
    Rais William Ruto

Rais William Ruto wa Kenya amesema serikali imetekeleza ahadi muhimu ilizotoa kwa jamii ya Waislamu wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2022.

Rais Ruto ametaja kukomeshwa mchakato wa ukaguzi wa kibaguzi katika utoaji wa vitambulisho vya taifa na pasipoti, pamoja na kuimarishwa ushirikishwaji katika maendeleo.

Amesema kuwa alisaini dikrii ya urais ililokomesha rasmi taratibu za ziada za ukaguzi zilizodumu kwa miongo kadhaa na ambazo kihistoria ziliwalenga zaidi Waislamu katika maeneo ya mipakani mwa nchi.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi jana Jumatano, alipowaalika viongozi wa dini ya Kiislamu, Rais William Ruto aliwahakikishia kuwa utekelezaji uliochelewa wa sheria kuhusu mali za wakfu za Kiislamu utakamilishwa ifikapo Septemba 2026.

Aidha, Rais Ruto amesema ujenzi wa korido ya barabara ya Isiolo–Mandera yenye urefu wa kilomita 750 unaendelea kwa mujibu wa mpango. Amesema mradi huo mkubwa wa miundombinu umeundwa kuunganisha jamii zilizotengwa kihistoria Kaskazini mwa Kenya na masoko makuu ya kiuchumi pamoja na huduma muhimu.

Ruto amesema atatoa mchango binafsi wa jumla ya shilingi milioni 70 za Kenya kusaidia juhudi za kulinda na kuendeleza majengo na miundombinu inayohusishwa na Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK) mjini Mombasa na magharibi mwa Kenya.

Kuhusu elimu, Rais Ruto amesema kuwa kuingizwa kwa elimu ya duksi na madrasa za Kiislamu katika mfumo rasmi wa elimu nchini ni ahadi nyingine ambayo serikali yake inaendelea kuitekeleza.

Pia amesema serikali imeimarisha mipango ya kuajiri na kutoa mafunzo kwa walimu katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya, ili kukabiliana na upungufu wa muda mrefu wa walimu na kupunguza usumbufu katika mchakato wa kujifunza.

Akijibu wito wa kutaka Mpango wa Nyumba za Bei Nafuu uzingatie misingi ya fedha ya Kiislamu, Rais Ruto amewahakikishia viongozi wa Kiislamu kwamba serikali yake tayari imeandaa mfumo utakaowawezesha Waislamu kupata nyumba kwa namna inayozingatia misingi ya Shariah.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Afya, Aden Duale, amesema Rais Ruto amehakikisha usawa katika ugawaji wa rasilimali na maendeleo katika maeneo yote ya nchi. Naye Katibu Mkuu wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), Omar Hassan, amesema uongozi wa Rais Ruto umeshughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Kenya.

Mkutano huo na maimamu, wanazuoni wa Kiislamu na viongozi wa jamii umetajwa kuwa wa kihistoria, kwa kuwa ulikuwa wa mara ya kwanza kwa mkusanyiko mkubwa kiasi hicho wa viongozi wa Kiislamu kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais wa Nchi.

Zaidi ya washiriki 8,000 kutoka kaunti zote 47 walihudhuria mkutano huo, ambapo waliwasilisha masuala yanayoathiri jamii zao pamoja na mapendekezo ya hatua za serikali.