Wanachama wawili wa kundi la kigaidi la Daesh wanyongwa nchini Iran
Wanachama wawili wa kundi la kigaidi la wakufurishaji la Daesh (ISIS), ambao walipatikana na hatia ya kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi na uasi wa kutumia silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, wamehukumiwa kifo na kunyongwa baada ya hukumu zao kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Iran.
Mohyeddin Abdollahi na Hossein Palani, waliotambuliwa kama wanachama wa kijitawi cha kundi kigaidi ya Daesh kilichoundwa baada ya kuporomoka kwa kundi hilo nchini Iraq na Syria na iliyokuwa imepanga mashambulizi ndani ya Iran, wamenyongwa leo Jumanne, Julai 14, kufuatia kukamilika kwa taratibu za kisheria na uthibitisho wa hukumu zao na mahakama ya ngazi ya juu ya Iran.
Vikosi vya usalama vya Iran viligundua maficho yao katika eneo la milima ya Bamo kwenye mpaka kati ya eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan ya Iraq na Iran, na kutoa pigo kali kwa magaidi hao.
Magaidi kadhaa waliuawa katika mapigano makali, na wanajeshi watatu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) walikufa shahidi katika operesheni hizo.
Magaidi wengine wa Daesh waliosalia walikamatwa, na maafisa wa usalama walinasa kiasi kikubwa cha silaha, risasi, vifaa, na nyaraka za siri.
Kufuatia taratibu za kisheria, ikiwemo kuwasilisha utetezi kutoka kwa watuhumiwa na mawakili wao, mahakama iliwatia hatiani watu hao wawili kwa kosa la uasi wa kutumia silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kuwahukumu kifo.
Mahakama Kuu baadaye ilipitia na kuthibitisha hukumu hizo, na utekelezaji wa adhabu hiyo ulifanyika baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika.