Araqchi: Iran iko tayari kukabiliana na uvamizi wowote mpya wa Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi ameonya dhidi ya kitendo chochote kipya cha uvamizi cha Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akisisitiza kwamba Tehran iko tayari kikamilifu kukabiliana na makosa yoyote kama hayo.
Abbas Araqchi alitoa matamshi hayo wakati wa mazungumzo yake tofauti ya simu na mwenzake wa Uturuki, Hakan Fidan, na Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Field Marshal Asim Munir jana Jumamosi.
Mazungumzo hayo yalijadili matukio ya hivi karibuni ya kikanda, ikiwa ni pamoja na athari za vitendo vya ukatili na vya kuyumbisha amani vya Marekani.
Wakati wa mazungumzo hayo, Araqchi ameeleza utayarifu kamili wa Jamhuri ya Kiislamu wa kulinda mamlaka yake ya kitaifa, ardhi yake na usalama, na kujibu kwa dhati kitendo chochote cha uchokozi.
Tangu tarehe 7 Aprili, Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran baada ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja katika mzozo wa hivi karibuni wa uchokozi usio na sababu wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Marekani pia imekuwa ikijaribu kuzisaidia meli kukwepa njia ya baharini iliyoainishwa na Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kupita salama katika Lango-Bahari la Hormuz.
Vikosi vya Jeshi la Iran vimelipiza kisasi kwa kushambulia kambi na vituo vya Marekani Magharibi mwa Asia, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na jaribio lolote la kupitisha meli katika Lango bahari la Hormuz bila ya idhini ya Iran.