Iran yaimarisha ‘Dhahabu ya Kijani’ licha ya njama za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136160-iran_yaimarisha_dhahabu_ya_kijani’_licha_ya_njama_za_marekani
Sekta ya njugu aina ya pistachio ya Iran kwa muda mrefu imekuwa nguzo muhimu ya mauzo ya nje ya kilimo ya nchi hii, ikiwa imejikita kwa kina katika uchumi na utamaduni wa Iran.
(last modified 2026-02-02T03:11:08+00:00 )
Feb 02, 2026 03:11 UTC
  • Iran yaimarisha ‘Dhahabu ya Kijani’ licha ya njama za Marekani

Sekta ya njugu aina ya pistachio ya Iran kwa muda mrefu imekuwa nguzo muhimu ya mauzo ya nje ya kilimo ya nchi hii, ikiwa imejikita kwa kina katika uchumi na utamaduni wa Iran.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), mauzo ya nje ya pistachio ya Iran yaliongezeka kwa asilimia 80 mwaka 2024, hatua iliyoiwezesha nchi hii kushika nafasi ya pili duniani, nyuma ya Marekani.

Katika kipindi hicho, Iran ilisafirisha tani 316,000 za pistachio kwenda masoko ya kimataifa, ongezeko kubwa linaloashiria kuimarika kwa sekta hiyo. Kwa kulinganisha, Marekani ilirekodi ongezeko dogo la asilimia 5 pekee katika mauzo yake ya nje, huku Uturuki ikipanua hisa yake ya soko kwa asilimia 40.

Pistachio, maarufu kama “dhahabu ya kijani” nchini Iran, ni zao muhimu la mauzo ya nje katika nchi ambayo kwa muda mrefu imejulikana kwa umahiri wake wa kilimo. Pistachio za Iran zinachukuliwa kuwa miongoni mwa bidhaa zisizo za mafuta zenye thamani kubwa zaidi, na si bila sababu.

Kuanzia nafasi ya kihistoria ya pistachio katika njia za biashara za kale kama Barabara ya Hariri, hadi kilimo chake kilichokita mizizi katika maeneo kama Kerman, Rafsanjan na Yazd, zao hili limekuwa sehemu isiyotenganishwa na utambulisho wa Iran.

Hata hivyo, soko la kimataifa la pistachio sasa limegeuka kuwa uwanja wa ushindani mkali, ambapo Marekani imetumia mbinu mbalimbali zisizo za haki kuimarisha nafasi yake huku ikidhoofisha kwa makusudi satwa ya kihistoria wa Iran katika sekta hiyo.

Katikati ya karne ya 20, Iran ilikuwa kinara asiye na mpinzani katika uzalishaji wa pistachio, ikidhibiti asilimia 75 ya mauzo ya pistachio duniani kufikia mwaka 1970. Wakati huo, Uturuki ndiyo ilikuwa mpinzani pekee, ikiwa na hisa ya soko ya takriban asilimia 25.

Mkakati wa Marekani ulianza katika miaka ya 1970 kwa kuagiza aina za pistachio kutoka Iran. Aina ya Kerman, inayotambuliwa kwa mapana kama aina bora zaidi ya pistachio duniani, ilisafirishwa kinyume cha sheria hadi Bonde la Kati la California na ikawa msingi wa uzalishaji wa pistachio wa Marekani.

Sekta ya pistachio ya California ilikua kwa kasi na kuwa mpinzani mkubwa katika masoko ambayo kwa muda mrefu yalitawaliwa na pistachio za Iran, ikishindana uso kwa uso na Iran katika masoko kama Japani, Asia ya Kusini Mashariki na Ulaya.

Hata hivyo, Iran inaendelea kushikilia sehemu muhimu ya soko la kimataifa, hususan barani Asia. China, India na Urusi zimeibuka kuwa masoko muhimu ya pistachio za Iran, hata wakati Marekani ikiendelea kujaribu kuimarisha ushawishi wake katika sekta hiyo.