Afisa wa Yemen: Hatujawahi katu kufunga milango ya mazungumzo na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140598-afisa_wa_yemen_hatujawahi_katu_kufunga_milango_ya_mazungumzo_na_saudia
Mkuu wa ujumbe wa Yemen katika mazungumzo ya amani amesema, Sana'a haijawahi kufunga milango ya mazungumzo na Saudi Arabia, bali Saudia ndiyo inayokataa suala hilo.
(last modified 2026-08-12T03:31:25+00:00 )
Aug 12, 2026 03:24 UTC
  • Muhammad Abdulsalam
    Muhammad Abdulsalam

Mkuu wa ujumbe wa Yemen katika mazungumzo ya amani amesema, Sana'a haijawahi kufunga milango ya mazungumzo na Saudi Arabia, bali Saudia ndiyo inayokataa suala hilo.

Muhammad Abdulsalam amefafanua kwa kusema: "sambamba na kuendelea uchokozi dhidi ya taifa letu, timu ya mazungumzo inaendelea kufanya mawasiliano na mikutano na pande mbalimbali ili kubainisha msimamo wetu kuhusu matukio yanayojiri. Operesheni za vikosi vyetu vya ulinzi dhidi ya meli za Saudi Arabia, mikusanyiko ya vikosi vyake na kambi zake za kijeshi ndani ya nchi ni sehemu ya majibu yetu halali kwa mashambulizi, likiwemo shambulio dhidi ya uwanja wa ndege wa Sana'a."

Abdulsalam ameongeza kuwa: "Sanaa imeheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kupunguza mivutano kwa muda wa miaka minne na haijachukua hatua yoyote ya uadui dhidi ya Saudi Arabia. Lakini kwa upande wake, Saudia imeitumia vibaya fursa ya kusitisha mapigano ili kushadidisha makusudi hali mbaya katika nyanja za kiuchumi na maisha ili kuliatilisha taifa letu."

Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Masirah, Abdul Salam ameendelea kueleza kwamba: "Saudi Arabia imeshadidisha mzingiro wa mabavu dhidi ya watu wetu kwa kuzikagua meli. Saudia imezilenga benki, maduka ya kubadilisha fedha na wafanyabiashara. Kuzilenga benki, maduka ya kubadilisha pesa na wafanyabiashara kumeifanya hali ya kibinadamu iwe mbaya zaidi. Kumeongeza gharama na kuwafanya watu wakabiliwe na ongezeko kubwa sana la bei za bidhaa.

Mohammed Abdulsalam amesisitiza kwa kusema: "hatujawahi katu kufunga milango ya mazungumzo; ni upande wa Saudia ndio unaokataa; msimamo uliotangazwa hivi karibuni umeweka wazi suala hilo na unapingana na madai yao ya kuunga mkono kutumia njia za amani za utatuzi. Saudi Arabia inafanya ucheleweshaji ili kufanikisha njama zake, maandalizi yake ya kijeshi na kuitumbukiza Yemen katika machafuko na vita visivyokwisha".

Mkuu wa ujumbe wa Yemen katika mazungumzo ya amani amesisitiza: "sambamba na kukabiliana na njama, vikosi vyetu vya ulinzi vinaendelea kutimiza wajibu wao wa kulinda mamlaka ya kujitawala, uhuru na heshima ya Yemen, na kudhamini haki kamili za wananchi. Tunasisitiza kwa pande za kikanda na kimataifa zinazoamiliana nasi kwamba, muelekeo wowote wa baadaye lazima upelekee kutambuliwa haki halali za watu wetu, kwanza kabisa ikiwa ni kufunguliwa tena viwanja vya ndege na bandari, kulipwa mishahara, na kuanza tena mauzo ya nje ya mafuta na gesi…/