Kiongozi Muadhamu: Kwa tawfiq ya Mwenyezi Mungu, tutampigisha magoti adui
-
Kiongozi Muadhamu: Kwa tawfiq ya Mwenyezi Mungu, tutampigisha magoti adui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu taifa hili litashinda njama zote na kumpigisha magoti adui.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo alipokutana hapa mjini Tehran na familia za mashahidi katika kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Twalib (AS) na hauli ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, SEPAH.
Akihutubia hadhara hiyo, Ayatullah Khamenei amesisitiza haja ya kusimama kidete dhidi ya maadui.
Ameeleza kwamba, kumtambua adui kiukweli ni mafanikio makubwa na kuongeza: "Watu waliona dhati ya Marekani wakati wa vita vya siku 12. Hata wale walioamini kwamba suluhisho la matatizo ya nchi ni kufanya mazungumzo na Washington, walidiriki kwamba katikati ya mazungumzo, serikali ya Marekani ilikuwa mashughuli kuandaa mpango wa vita."
Akizungumzia mashinikizo ya maadui kwa taifa la Iran, Kiongozi Muadhamu amesema: "Ni muhimu mtu anapohisi kwamba adui anataka kulazimisha matakwa yake kwa nchi na maafisa, kwa serikali na taifa, anapaswa kusimama kwa nguvu zote dhidi ya adui na kukinga kifua chake. Hatutarudi nyuma mbele ya adui. Inshaa Allah, tutampigisha magoti adui, kwa kumtegemea Mungu Mwenyezi, kwa kujiamini na kwa msaada wa wananchi."
Ayatullah Khamenei ameashiria maandamano ya baadhi ya wananchi hapa Iran na kubainisha kwamba, kuandamana na kupaza sauti ya malalamiko ni mahala pake, lakini kuandamana ni tofauti na kufanya machafuko. "Tunazungumza na waandamanaji, na wanapaswa kuzungumza na kueleza malalamiko yao. Lakini hakuna faida kwa maafisa wa serikali kuzungumza na waendesha machafuko. Mfanya machafuko anapaswa kuwajibishwa" amesisitiza Sayyid Ali Khamenei.