Hali ya Tigray nchini Ethiopia yamtia wasiwasi mkubwa Katibu Mkuu wa UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136156-hali_ya_tigray_nchini_ethiopia_yamtia_wasiwasi_mkubwa_katibu_mkuu_wa_un
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema anafuatilia kwa karibu kinachoendelea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, ambako mvutano unaoibuka upya na taarifa za mapigano vimechangia kuzorota kwa hali ya usalama.
(last modified 2026-02-02T03:08:40+00:00 )
Feb 02, 2026 03:08 UTC
  • Hali ya Tigray nchini Ethiopia yamtia wasiwasi mkubwa Katibu Mkuu wa UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema anafuatilia kwa karibu kinachoendelea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, ambako mvutano unaoibuka upya na taarifa za mapigano vimechangia kuzorota kwa hali ya usalama.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, Guterres ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba raia, pamoja na hatari ya kurejea kwa mzozo mpana katika eneo hilo ambalo lingali linaendelea kujijenga na kupona baada ya machafuko ya awali.

Katika taarifa hiyo, Haq amesema Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote zinazohusika kujizuia na kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo ya amani, pamoja na kuchukua hatua zitakazosaidia kujenga upya imani. 

Amesisitiza pia umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu Makubaliano ya Kudumu ya Kusitisha Mapigano, akibainisha umuhimu wa kulinda mafanikio yaliyopatikana tangu mwaka 2022.

Aidha, Katibu Mkuu amethibitisha utayari wa Umoja wa Mataifa kushirikiana na Umoja wa Afrika pamoja na washirika wa kikanda ili kusaidia kuimarisha amani na utulivu wa kudumu katika eneo la Tigray.

Mzozo huko Tigray unahusisha jeshi la serikali ya Ethiopia na kikosi cha wapiganaji cha Tigray, TPLF, na ulianza mwezi Novemba mwaka 2020 baada ya jeshi la serikali kudai kuwa wapiganaji hao wa Tigray walishambulia kituo cha jeshi la serikali. Miongoni mwa matakwa ya Tigray ni kujitenga na Ethiopia.

Hata hivyo mwezi Novemba mwaka  2022 Sitisho la Kudumu la Mapigano kati ya pande hizo mbili ilitiwa Saini huko Pretoria nchini Afrika Kusini kati ya serikali ya Ethiopia na TPLF.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, hali ya sasa inafuatia ripoti kwamba ndege zisizo na rubani zimeshambulia eneo la Tigray na kusababisha madhara katika eneo hilo.../