Hamas: Israel isitishe jinai ili mapatano ya usitishaji vita Gaza yafanikiwe
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, katika Ukanda wa Gaza amesisitiza kuwa harakati za Palestina zimejitolea kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kwamba mafanikio ya mapatano hayo sasa yanategemea kulazimishwa utawala haramu wa Israel kuyazingatia na kujiepusha na jinai inazoendeleza dhidi ya Wapalestina.
Kauli hiyo ya Khalil al-Hayya, iliyotolewa jioni ya Jumamosi, imekuja wakati uongozi wa Hamas ukiwa umeanzisha mawasiliano ya kina na wapatanishi pamoja na wadau wengine wa kimataifa. Katika mawasiliano hayo, kundi hilo limekataa vikali na kulaani mwenendo wa Israel pamoja na kuendelea kwa mashambulizi yake dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Al-Hayya amesema kuwa Hamas imesisitiza kuwa Israel inabeba jukumu kamili kwa kushindwa kufikiwa kwa suluhu kuhusu suala la wapiganaji wa Kiislamu au Muqawama walioko Rafah, ambao wamejipanga katika eneo lililo chini ya udhibiti wa kijeshi wa Israel.
Katika mawasiliano yake na wapatanishi pamoja na wadau wa kimataifa, Hayya ameonya kuhusu athari za uhalifu na mauaji ya halaiki yanayotekelezwa karibu kila siku na majeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, sambamba na ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesisitiza umuhimu wa kulazimisha Israel kusitisha ukiukaji huo. Hamas imepinga vikali madai ya Israel kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya mabomu huko Gaza ni “majibu” ya madai ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na harakati za mapambano ya Kiislamu (Muqawama). Hamas imesisitiza kuwa madai hayo “si chochote ila jaribio la wazi na la kusikitisha la kuhalalisha mauaji ya kutisha dhidi ya raia” katika ukanda huo wa pwani.
Ofisi ya Habari ya Gaza ilitangaza Jumamosi kwamba, tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana, mashambulizi ya Israel yameua Wapalestina 524 na kuwajeruhi wengine 1,360. Aidha utawala wa Israel umekiuka mapatano hayo mara 1,450.
Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yalihitimisha vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya vilivyodumu kwa miaka miwili. Tokea mauaji hayo yaanze Oktoba 7 2023, Israel imeua takriban Wapalestina 71,800 na kuwajeruhi zaidi ya 171,480.
Kampeni hiyo ya umwagaji damu imeharibu karibu asilimia 90 ya miundombinu ya kiraia katika eneo hilo la pwani, huku makadirio ya Umoja wa Mataifa yakionyesha kuwa gharama za ujenzi upya zinafikia takriban dola bilioni 70.