Afrika Kusini yamtimua Kaimu Balozi wa Israel
Afrika Kusini imemtangaza kaimu balozi wa utawala wa Isarel nchini humo kuwa mtu asiyehitajika na kuamuru aondoke mara moja.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imetangaza kuwa nchi hiyo inamfukuza mjumbe huyo wa Israel aliyekuwa akihudumu nchini humo, kutoka na kujihusisha na kile ilichokitaja kuwa ni “ukiukwaji usiokubalika wa misingi na kanuni za diplomasia,” vitendo ambavyo, kwa mujibu wa wizara hiyo, vinadhoofisha mamlaka ya Afrika Kusini kama taifa huru.
Hatua hiyo imekuja katika mazingira ya mvutano unaozidi kuongezeka kati ya Pretoria na Tel Aviv, huku Afrika Kusini ikisisitiza dhamira yake ya kulinda heshima ya taifa, misingi ya diplomasia ya kimataifa, na uhusiano unaojengwa kwa kuheshimiana.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ilisema kuwa kuanzia Ijumaa ilimpa Ariel Seidman, kaimu balozi (chargé d’affaires) katika ubalozi wa Israel, muda wa saa 72 kuondoka Afrika Kusini baada ya kumtangaza kuwa persona non grata yaani mtu asiyehitajika.
Wizara hiyo ilimtuhumu Seidman kwa kufanya “mashambulizi ya matusi” dhidi ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kupitia mitandao ya kijamii, pamoja na kile ilichokitaja kuwa ni “kushindwa kwa makusudi” kuijulisha wizara hiyo kuhusu “ziara za maafisa waandamizi wa Israel” nchini humo.
Tangazo hilo lilizua majibu ya haraka kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ambayo ilisema kuwa nayo imemtangaza kumtimua mwanadiplomasia mwandamizi wa Afrika Kusini, Shaun Edward Byneveldt, na kumpa muda wa saa 72 kuondoka katika utawala wa 'Israel'.
Kwa mujibu wa tovuti ya serikali ya Afrika Kusini, Shaun Edward Byneveldt ni balozi wa Afrika Kusini katika Dola ya Palestina, akifanya kazi kutoka ofisi iliyopo Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Chrispin Phiri, alisema kuwa “vizingiti na ubishi wa Israel vimeilazimisha hali ya kuchekesha ambapo [Byneveldt] analazimika kuidhinishwa kupitia utawala ule unaokalia kwa mabavu nchi anayowakilisha.”
Hatua hizi za kulipizana kisasi kidiplomasia zimekuja wakati mvutano kati ya Afrika Kusini na Israel ukiendelea kuongezeka kwa miezi kadhaa, kufuatia vita vya mauaji ya kimbari vya Isarel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Mwisho wa Desemba 2023, Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikiituhumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari katika eneo hilo linaloshambuliwa vikali.