Wanazuoni wa Yemen watangaza mshikamano na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i136154-wanazuoni_wa_yemen_watangaza_mshikamano_na_iran
Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imetangaza mshikamano wake kamili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutaka ulimwengu wa Kiislamu kuchukua msimamo wa pamoja katika suala hilo.
(last modified 2026-02-02T02:42:32+00:00 )
Feb 02, 2026 02:42 UTC
  • Wanazuoni wa Yemen watangaza mshikamano na Iran

Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imetangaza mshikamano wake kamili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutaka ulimwengu wa Kiislamu kuchukua msimamo wa pamoja katika suala hilo.

Jumuiya hiyo imesisitiza uungaji mkono wake kamili kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na imewataka wanazuoni wa ulimwengu wa Kiislamu kutangaza msimamo wa kindugu wa Kiislamu kuunga mkono Tehran dhidi ya mashinikizo ya Marekani na utawala wa Israel, tovuti ya Naba iliripoti.

Imeeleza umuhimu wa uthabiti na msimamo wa upinzani, na kuonya dhidi ya kutoa mwanya wowote kwa madai ya Marekani, utawala wa Israel na nchi za Magharibi.

Jumuiya hiyo pia imesisitiza haja ya kuonyesha uaminifu kwa waumini na kuchukua msimamo wa wazi dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu.

Vilevile, imeutaka ulimwengu wa Kiislamu hasa serikali, mataifa na majeshi kuacha ukimya na kutoegemea upande wowote unaoonekana kuwa wa aibu, ikisisitiza kuwa changamoto zinazokabili ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla na Iran kwa hususan zinahitaji msimamo wa pamoja na wenye ufanisi.

Katika hitimisho la taarifa yake, jumuiya hiyo imetoa wito wa uhamasishaji wa umma, kuongeza viwango vya utayari, na kuitikia mwito wa Qur’ani wa kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu, ikisisitiza kuwa hatua ya sasa inahitaji mshikamano na kuchukua misimamo ya vitendo inayozidi matamko ya kulaani pekee.

Taarifa hiyo inakuja wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, akiongeza makali ya matamshi yake, akitishia kuchukua hatua mpya za kijeshi dhidi ya Iran.

Hivi karibuni, Washington ilipeleka manowari ya kubeba ndege za kivita, USS Abraham Lincoln, pamoja na kikosi chake cha mashambulizi, katika eneo la Asia Magharibi karibu na Iran.

Maafisa wa Iran wameonya kuwa kutakuwa na majibu makali ya kijeshi endapo kutafanyika kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya nchi hiyo.