2025, mwaka wa kushindwa uchumi wa Marekani
-
Kuporomoka uchumi wa dunia katika mwaka 2025
Gazeti la Marekani la Axios limeandika kuwa: Katika mwaka uliomalizika majuzi wa 2025, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza wa urais wa Donald Trump, uchumi wa Marekani ulifika kwenye ukingo wa mgogoro kutokana na mfumuko wa bei, kupungua kwa ajira, na kutoridhika kwa umma.
Gazeti la Axios limeutaja mwaka 2025 kuwa ulikuwa "mwaka ambao uchumi wa Marekani ulielekea ukingoni mwa kuporomoka" lakini Trump mwenyewe anaendelea kudai kwamba utendaji wake wa kiuchumi umekuwa bora, japo waangalizi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi nchini Marekani wanatambua madai hayo kuwa hayana msingi.
Katika suala hili, Jason Johnson, mtangazaji wa MS Now TV, amesema: "Katika dunia halisi, kinyume na madai ya Trump, zaidi ya theluthi mbili ya Wamarekani, au asilimia 68, wanasema kwamba hali ya kiuchumi ya nchi inazidi kuwa mbaya, hii ni pamoja na kuwa, kutokana na kuboronga kwa Trump na timu yake, bima ya afya ya Wamarekani wapatao milioni 20 inatarajiwa kusitishwa kuanzia mwanzoni mwa huu wa 2026."
Wakati huo huo, Marjorie Taylor Greene, mbunge aliyejiuzulu wa Bunge la Marekani, amejibu madai ya Trump kwamba matumizi ya serikali kwa ajili ya wananchi yanafaa, akisema: "Trump anapaswa kuelewa kwamba yeye ni bilionea. Huwezi kuwadanganya watu na kuwaambia kwamba matumizi yao ni ya gharama nafuu na kwamba uchumi wa Marekani unafanya vizuri, kwa sababu sivyo ilivyo hata kidogo."
MarketWatch, tovuti ya kuchambua data zinazohusiana na soko la hisa la Marekani, inayohusishwa na Wall Street Journal, pia imeandika kwamba: "Kwa mtazamo wa wananchi wa Marekani, uchumi wa nchi ni mbaya sana, na ushuru, mfumuko wa bei na kupungua kwa ajira vilikuwa miongoni mwa sifa kuu za uchumi wa Marekani mwaka uliomalizika wa 2025."
Kwa upande wake, Anthony Salvanto, mkurugenzi wa kitengo cha uchambuzi cha televisheni ya CBS, ameripoti kwamba: "Kiwango cha kuridhika wananchi kutokana na utendaji wa kiuchumi wa Trump mwaka 2025 kimekuwa kikishuka kutoka asilimia 51 hadi asilimia 37, na hapana shaka kwamba kitaendelea kupungua katika mwaka mpya. Kura za maoni zinaonyesha kwamba serikali imefanya vibaya sana katika suala la kupunguza mfumuko wa bei na matumizi."
Katika mkondo huo huo, mwanaharakati wa uchumi wa Marekani, Tara Setmayer pia amesisitiza kuwa: "Donald Trump hawajali kabisa Wamarekani wa kawaida na hampi umuhimu mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe."
Wachambuzi wa mambo wanasisitzia kuwa, kipindi cha urais wa Donald Trump kimeandamana na usaliti wa PDP kwa watu wa kawaida na hata wale waliompigia kura. Wanasema, amewasaliti Wamarekani wote, kuanzia familia za wakulima na wanajeshi, maveterani, wamiliki wa biashara ndogo ndogo hadi wafanyakazi wa Marekani, na katika kipindi hicho chote amezidisha utajiri wake na kutumia vibaya pesa za walipa kodi wa Marekani.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, katika kipindi cha takriban mwaka mmoja tu, utajiri wa Trump umeongezeka kwa zaidi ya dola bilioni 3. Hii ni licha ya kwamba kwa sasa, Wamarekani wengi wanateseka kutokana na matatizo ya kiuchumi na wanaishi kwa wasiwasi na misukosuko.