Hizbullah: Iran haijataka chochote kwetu mkabala wa kutusaidia, kutuunga mkono
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135104-hizbullah_iran_haijataka_chochote_kwetu_mkabala_wa_kutusaidia_kutuunga_mkono
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem amepongeza ustadi wa kijeshi wa aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Luteni Jenerali Qassem Soleimani na kuongeza kuwa, Iran haijataka chochote kutoka kwa harakati hiyo ya Muqawama mkabala wa uungaji mkono wake kwake.
(last modified 2026-01-04T11:06:13+00:00 )
Jan 04, 2026 11:06 UTC
  • Hizbullah: Iran haijataka chochote kwetu mkabala wa kutusaidia, kutuunga mkono

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem amepongeza ustadi wa kijeshi wa aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Luteni Jenerali Qassem Soleimani na kuongeza kuwa, Iran haijataka chochote kutoka kwa harakati hiyo ya Muqawama mkabala wa uungaji mkono wake kwake.

Sheikh Naim Qassem amesema hayo katika hotuba aliyotoa kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka sita ya kuuawa shahidi Jenerali Qassem Soleimani na Hajj Abu Mahdi Al-Muhandis.

Tovuti ya Al-Manar TV inayotangaza kwa lugha ya Kiingereza imemnukuu Sheikh Qassem akiwapongeza Waislamu kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Imam Ali (AS) iliyoadhimishwa jana na kusema: Mwenyezi Mungu ametubariki kwa uaminifu kwa Amirul-Muuminin.

Aidha amesema "Shahid Soleimani alikuwa kiongozi wa kijeshi mwenye mawazo ya kipekee na ujuzi wa aina yake, na ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na Bwana wa Mashahidi wa Umma Sayyid Hasan Nasrullah. "Lengo kuu la Shahidi Suleimani lilikuwa kuunga mkono upinzani wa Wapalestina dhidi ya adui wa Israel."

"Kuuawa kwa Shahidi Soleimani kuliimarisha tena njia ya Muqawama," amesema mwanachuoni huyo wa Lebanon na kuongeza kuwa, "Mauaji ya mashahidi hayatazuia kustawi kwa mrengo wa Muqawama katika eneo hili."

Sheikh Qassem ameendelea kusema kwamba, "Magharibi ilipandikiza 'Israel' huko Palestina ili kudumisha ushawishi wa kielimu na kiuchumi katika eneo la Asia Magharibi.

Kiongozi wa Hizbullah ameashiria uchaguzi wa Lebanon na kusema kuwa, "Hizbullah inatoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi wa bunge la Lebanon kama ilivyopangwa." Hali kadhalika amesema, "Hizbullah inatoa wito wa kulipatia Jeshi la Lebanon silaha zinazofaa ili kuilinda Lebanon na kudumisha utulivu wa ndani."